Habari

Joto la siasa linafukuza wawekezaji – Atwoli

October 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Cotu, Bw Francis Atwoli amesema kwamba joto la kisiasa linaloendelea kupanda nchini linawatia hofu wawekezaji ambao wamewaajiri maelfu ya Wakenya.

Bw Atwoli alisema kwamba wawekezaji wamekuwa wakihamia nchi nyingine wakihofia fujo za kisiasa.

“Wafanyakazi wanaumia. Wawekezaji wamehamisha biashara za thamani ya Sh60 bilioni kwa sababu wanahofia joto la kisiasa nchini ingawa uchaguzi uko mbali,” Bw Atwoli alisema.

Wanasiasa wamekuwa wakiandaa mikutano ya kisiasa inayovutia idadi kubwa ya watu ambapo wamekuwa wakilaumiana hasa kuhusu pendekezo la kurekebisha katiba na siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Watu wawili walifariki Kaunti ya Muranga wafuasi wa mirengo miwili ya chama cha Jubilee walipokabiliana wakati wa mkutano wa Naibu Rais William Ruto mjini Kenol wiki tatu zilizopita.

Bw Atwoli alisema wanasiasa wanafaa kusubiri Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakapotoa idhini ya kampeni za kisiasa.

“Sisemi wanasiasa wasishiriki mikutano. Sisemi watu wasitekeleze haki yao ya kuandaa mikutano ya kisiasa. Ninachosema ni kwamba ni mapema mno kwa siasa ambazo zimefanya wawekezaji kuondoka Kenya. Wakati wa kampeni utafika lakini kwa sasa tuzingatie kuimarisha uchumi wetu ili kulinda nafasi za ajira na kubuni mpya,” alisema Bw Atwoli akizungumza na runinga ya NTV akiwa nyumbani kwake Kajiado.

Alisema ingawa anaunga mkono kura ya maamuzi ya kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), kampeni zinafaa kuanza tu IEBC ikitoa idhini.

“Hata kampeni za BBI ambayo ninaunga, tunafaa kusubiri IEBC itupatie kalenda kabla ya kuanza kampeni,” alisema Bw Atwoli.

Alisema amehimiza IEBC kutoa kalenda ya kampeni ili kusitisha joto la kisiasa nchini.

“Kuna wasiwasi mwingi kwa sababu ya matamshi ya kisiasa tunayoshuhudia, yanaweza kuchochea Wakenya na hii inaweza kuathiri uchumi,” alisema.