• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
DIMBA: Haaland ni silaha hatari katika ufungaji mabao

DIMBA: Haaland ni silaha hatari katika ufungaji mabao

Na GEOFFREY ANENE

ERLING Braut Haaland ni mmoja wa makinda matata wanaoorodheshwa juu katika ulimwengu wa katika idara ya ushambuliaji wakati huu.

Mzawa huyu wa Uingereza anayefahamika kwa jina la utani kama ‘Manchild’ amekuwa akimezewa mate na ‘mashetani wekundu’ wa Manchester United kwa muda sasa.

Braut, ambaye ni mchezaji wa Borussia Dortmund kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, alizaliwa Julai 21 mwaka 2000.

Raia huyu wa Norway alizaliwa mjini Leeds nchini Uingereza wakati babaye Alf-Inge Haaland alikuwa mchezaji wa Leeds United.

Alf-Inge, ambaye pia alichezea Manchester City, alichangia pakubwa katika soka ya Braut kwa kumpatia msingi mzuri wa mazoezi na nidhamu. Braut ni mtoto wa pili wa Alf-Inge na mamaye Gry Marita.

Braut alipenda soka, gofu, riadha na handiboli akiwa mtoto alipokuwa akilelewa mtaani mwake Bryne nchini Norway.

Aliamua kutupilia mbali fani hizo zingine na kuzamia soka akiwa na umri mdogo wa miaka sita pekee alipojiandikisha katika timu ya Bryne Fotballklubb.

Akiwa Bryne, Braut aliweka malengo yake ya juu akitumainiwa kuwa siku moja atakuwa mchezaji bora duniani. Ripoti nchini Norway zinasema kuwa alikuwa tayari kufanya kila kitu alichohitajika kufanya ikiwemo kuingia katika chumba cha kufanyia mazoezi ya viungo ili kutimiza ndoto yake.

Akiwa mtoto, Haaland alisakata soka ya kupendeza. Kufikia umri wa miaka 15, alikuwa anafuatwa na maskauti kila alipojibwaga uwanjani.

Hatua yake ya kwanza kubwa katika uchezaji wake ilikuwa mwaka 2018 wakati alisaini kandarasi na Red Bull Salzburg akitokea Molde nchini Norway alikokuwa na msimu wa kufana.

Tangu wakati huo, Haaland amejitokeza kuwa mmoja wa wachezaji wanaoaminika silaha hatari katika ufungaji wa mabao. Kupitia talanta yake ya hali ya juu na pia anavyosherehekea magoli, Haaland amepata umaarufu mkubwa.

Alipiga hatua nyingine kubwa maishani alipojiunga na mojawapo ya ligi kubwa barani Ulaya na dunia aliposajiliwa na Borussia Dortmund mnamo Desemba 2019 kucheza kwenye Bundesliga.

Alinunuliwa na Dortmund kwa Yuro 20 milioni akisaini kandarasi itakayomweka katika klabu hiyo hadi mwaka 2024. Mojawapo ya sababu zake za kujiunga na Dortmund ni kuwa klabu hiyo inafahamika sana katika kusaidia makinda kuimarisha soka yao.

Haaland anaenzi mchana nyavu matata Zlatan Ibrahimovic.

Mswidi Ibra ni mmoja wa wachezaji wanaofanya ajitume zaidi mazoezini na uwanjani. Mbali na kazi yake kutambulika uwanjani, Haaland amekuwa sumaku ya matangazo ya kibiashara.

Kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike kutoka Amerika imekuwa ikishirikiana naye kunadi bidhaa zake. Amesaini kandarasi na kampuni hiyo inayomletea donge nono.

Mchezaji huyu amekuwa akimezewa mate na klabu kubwa. Amekosesha usingizi miamba wa Uhispania Real Madrid na Waingereza Manchester United, ambao wamehusishwa naye kwa muda mrefu. Tovuti ya wtfoot inasema ukwasi wa Haaland umefika Yuro milioni nne, ingawa thamani yake sokoni inakadiriwa kupanda kutoka Yuro milioni tano mapema mwaka 2019 hadi Yuro 80 milioni wakati huu.

You can share this post!

Demu ‘sumaku’ afukuzwa ploti

MBWEMBWE: Ukwasi wa Sergio utagharimia karo vyuoni Kenya...