• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Walimu wa elimu ya dini waanza mikakati ya kufungua vyuo na taasisi

Walimu wa elimu ya dini waanza mikakati ya kufungua vyuo na taasisi

Na MISHI GONGO

WALIMU wa taasisi na vyuo mbalimbali vya elimu ya dini mjini Mombasa wameanza mikakati ya kufungua vyuo hivyo baada ya kufungwa kwa miezi saba kutokana na janga la corona.

Walimu hao walisema wanapanga kufungua vyuo hivyo Juma lijalo kuanza masomo rasmi, wakisisitiza kuwa kuna haja ya kurudi mafundisho ya dini kukabili utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi.

Akizungumza na Taifa Leo hapo Jumapili mwalimu wa madrasa Answar Kisauni Ustadh Ali Hamid alisema wameweka mikakati kuhakikisha kuwa watoto wako salama.

Walisema hayo ikiwa ni wiki moja baada ya serikali kufungua shule.

“Tumeweka matayarisho kuhakikisha kuwa tunatekeleza masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa hatuhatarishi hali za kiafya za wanafunzi,” akasema.

Mwingine, ustadha Aisha Badru alisema kuwa tangu kufungwa kwa vyuo hivyo watoto wameanza kupotoka kimaadili.

Alieleza kuwa muda walioketi nyumbani kufuatia kuzuka kwa janga la corona, wametagusana na watu wenye tabia mbalimbali wakiwemo watumizi wa dawa za kulevya.

“Watoto hufaa kupewa mafunzo ya kuwa na maadili mema. Wanapoachwa huru ni rahisi kwao kupotoshwa; hivyo tunataka kuwarudisha,” akasema ustadha huyo.

Walizidi kuomba serikali iwarusuhu kuendeleza masomo.

Mwalimu wa madrasa moja Magongo Fadhili Thabit alisema kufuatia kufungwa kwa madrasa watoto wengi wamekuwa wakirandaranda mitaani huku wakitelekeza masomo ya dini.

Aliwasharauri wazazi kuwarudisha watoto wao madrasa.

Aidha alisema watoto wengi wamesahau mafunzo waliokuwa wakipewa.

Mwalimu mwingine Ibrahim Pesa, aliwahimiza wazazi kutumia teknolojia kuwafundisha watoto wao.

Walisema kuwa miongoni mwa matayarisho waliyoyafanya kuhakikisha usalama wa watoto ni kuvalia barakoa, kuweka maji na sabuni ya kutosha kuhakikisha kuwa watoto wanadumisha usafi wa kutosha.

Pia walisema watahakikisha wanafunzi wanaingia kwa zamu na kwa awamu tofauti ili kuhakikisha watoto hawakongamani.

“Tutaweka makundi mawili ambapo baadhi watakuwa wanaingia asubuhi huku wengine wakiingia mchana ili kuhakikisha kuwa kuna nafasi ya kutosha watoto kuekeana umbali unaostahili,” akasema Pesa.

Bi Stacey Mruche kutoka kanisa la Sayuni ambaye ni mwalimu wa kuwafundisha watoto mafunzo ya kanisa, alisema kuwa wameanza kuwafundisha watoto.

Alisema wanafuatilia vigezo vyote kuhakikisha kuwa wanalinda hali za kiafya za wanafunzi.

You can share this post!

Mbunge Ali Mbogo awataka wasichana wa shule wajiepushe na...

Wakazi wa Mwakirunge kupata hatimiliki