HabariSiasa

Waziri wa zamani ajifungia nyumbani asikamatwe na EACC

May 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na FRED MUKINDA

MAKACHERO wa Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) wanamsaka aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Michael Kamau baada ya kukosa kumkamata katika msako waliofanya nyumbani kwake Jumanne.

Kulingana na Naibu Afisa Mkuu wa EACC, Michael Mubea, maafisa hao walishindwa kumkamata Bw Kamau kwani alijifungia ndani ya nyumba na akakataa kuwafungulia maafisa hao walipowasili katika makazi ya Windy Ridge mtaani Karen.

“Tulienda kwake kumkamata ili ahojiwe kisha afikishwe mahakamani. Hata hivyo alijifungia ndani na kukataa kutoka nje. Sisi si wale wanaovunja nyumba za watu. Niliwaambia maafisa wangu waondoke kwa kuwa tuna njia nyingi za kushughulikia suala hili,” akasema Bw Mubea.

Alieleza hatua hiyo ilitokana na kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji alipitia faili ya kesi ya waziri huyo wa zamani na alitoa idhini ya kukamatwa kwake Ijumaa iliyopita.

Jamaa wa familia ambaye hakutaka jina lake linukuliwe alieleza Taifa Leo kwamba makachero 10 waliokuwa ndani ya magari mawili waliwasili nyumbani mwa Bw Kamau saa kumi na moja alfajiri asubuhi na kuondoka saa nne mchana.

Hata hivyo mawakili wa Bw Kamau waliokita kambi nyumbani kwake walisimulia vinginevyo. “Makachero ambao hawakujitambulisha waliwasili katika makazi yake kwa lengo la kumnasa na kumhoji.

Mwenzangu Wanja Wambugu alifika na kuwaeleza kuna amri ya Mahakama ya Rufaa ya Julai mwaka 2017 iliyozuia uchunguzi dhidi yake,” akasema wakili Nelson Havi.

Tume ya EACC awali ilimchunguza Bw Kamau na akashtakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na ukiukaji wa kanuni za zabuni katika kandarasi ya ujenzi wa barabara.

 

Kujinusuru kortini 

Baadaye Bw Kamau alienda kwenye Mahakama Kuu akilenga kuzuia kesi dhidi yake akihoji kwamba tume ya EACC haikuwa na idadi inayotakikana ya makamishna alipofikishwa mahakamani.

Ingawa Mahakama Kuu ilikataa kuzuia kushtakiwa kwake, alikimbilia Mahakama ya Rufaa na majaji watatu wa mahakama hiyo wakafutilia mbali uamuzi wa korti ya hakimu. Uamuzi huo ulisababisha mahakama hiyo ya chini kumwachilia.

Waziri huyo wa zamani tena alikimbilia Mahakama Kuu akidai mahakama ya hakimu ingemwondolea kesi kabisa badala ya kumwaachilia lakini mwezi Aprili mahakama hiyo ilikataa pendekezo lake na kuiruhusu EACC ianze uchunguzi mpya dhidi ya madai ya kushiriki ufisadi yanayomkabili.

Pia Jaji wa Mahakama Kuu Hedwig Ongudi alikataa maombi yake ya kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.

“Mahakama ya rufaa haikumwaachilia kwa sababu yeye anadai kwamba alikamatwa kama tume haikuwa na makamishna wa kutosha. Sasa wapo na kesi iendelee. Madai ya mawakili wake ni propaganda tupu,” akasema Bw Mubea.

Wakili Havi alisema makachero hao walisema walipata maagizo kutoka juu kufanya upekuzi katika nyumba ya Bw Kamau lakini hata baada ya kuruhusiwa kufanya hivyo walionekana kuwa na malengo tofauti.

Aidha alilamika kwamba EACC inalenga kukiuka sheria na amri za mahakama katika kumshtaki waziri huyo wa zamani.