• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Pigo Liverpool Van Dijk akihofiwa kusalia nje kwa msimu mzima kutokana na jeraha

Pigo Liverpool Van Dijk akihofiwa kusalia nje kwa msimu mzima kutokana na jeraha

Na MASHIRIKA

BEKI matata wa Liverpool, Virgil van Dijk, amesema atapania kurejea ugani kwa matao ya juu zaidi baada ya kuarifiwa kwamba atahitaji kufanyiwa upasuaji wa goti.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 29 alipata jeraha kwenye gozi la wikendi lililoshuhudia Liverpool wakilazimishiwa sare ya 2-2 na Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Goodison Park.

Van Dijk alikabiliwa visivyo na kipa Jordan Pickford na ikabidi aondolewe ugani katika dakika ya 11 na nafasi yake kutwaliwa na difenda Joe Gomez. Ingawa haijulikani atasalia mkekani hadi lini, Liverpool wanahofia kwamba huenda nyota huyo akakosa mechi zote zilizosalia msimu huu.

“Jeraha la Van Dijk ni baya na kutokuwepo kwake kwa muda mrefu ni pigo kubwa kwa Liverpool. Huenda asalie nje hadi mwisho wa muhula japo tunasubiri tathmini ya madaktari baada ya upasuaji,” akasema kocha Jurgen Klopp kumhusu difenda huyo wa zamani wa Celtic na Southampton.

Tangu ashawishike kubanduka Southampton kwa Sh10.5 bilioni mnamo Januari 2018, Van Dijk amekuwa nguzo muhimu ugani Anfield na alisaidia Liverpool kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika msimu wa 2017-18 na pia katika EPL msimu wa 2018-19, kabla ya kutwaa mataji ya mashindano hayo misimu iliyofuata ya 2018-19 na 2019-20 mtawalia. Liverpool walinyanyua pia ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2019.

Hadi alipopata jeraha katika gozi la Merseyside dhidi ya Everton, sogora huyo raia wa Uholanzi alikuwa amechezea Liverpool mara saba katika mechi zote za msimu huu wa 2020-21.

Kutokuwepo kwa Van Dijk kambini mwa Liverpool kutamsaza kocha Jurgen Klopp katika ulazima wa kutegemea zaidi maarifa ya Gomez na Joel Matip pamoja na chipukizi Nathaniel Phillips, Rhys Williams na Sepp van den Berg.

Gomez na Matip hawajawahi kupangwa pamoja katika kikosi cha kwanza cha Liverpool tangu Oktoba 2017 kwenye mechi iliyoshuhudia wakipokezwa kichapo cha 4-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur uwanjani Wembley.

Ni matarajio ya kocha Frank de Boer wa timu ya taifa ya Uholanzi kuwa Van Dijk atakuwa amepona vilivyo kwa minajili ya fainali za Euro ambazo sasa zimeahirishwa hadi Juni 11 – Julai 11, 2021.

You can share this post!

Wakazi wa Mwakirunge kupata hatimiliki

AFYA NA ULIMBWENDE: Ujauzito haumaanishi kupoteza mvuto