Mahakama yaamuru Sudi arudishiwe walinzi
NA FAUSTINE NGILA
Mahakama ya Nakuru imeamuru serikali kurudisha walinzi wa mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi.
Hakimu mkuu Isaac Orenge alisema Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai alikiuka sheria kwa kumwondolea maafisa wa usalama mbuge huyo.
Hakimu huyo alisema Bw Sudi anapaswa kuwa na maafisa wa usalama kwani yeye ni mbunge. Alisema pia mbunge huyo hakufanyiwa haki.
“Mkuu huyo wa polisi anaagizwa kurudishia mbunge huyo maafisa wa usalama alisema,” Bw Orenge alisema.
Bw Sudi ambaye anakabiliwa na makosa ya kutoa maneno ya chuki alienda kortini Jumanne kuomba kurudishiwa maafisa wa usalama wake.
Kupitia kwa mwanasheria wake Kipkoech Ng’etich Bw Sudi aliamboa korti kwamba maafisa wake wa usalama walitolewa Septemba 14 wakati walikamatwa na kufikishwa mahakamani Nakuru.
Bw Ng’etich alisema kwamba jambo hilo lilimuachwa mbunge huyo bila usalama wowote huku jambo hilo likiweka Maisha yake hatarini.
Masaibu ya Bw Sudi yalianza Septemba 7 wakati alitoa maneno ya chuki kwa familia ya Kenyatta.
Alijiwasilisha kwa polisi maeneo ya Langas baada ya kutafutwa kwa siku mbili na baadaye kuachiliwa kwa dhamana ya Sh 500,000.