• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Weita mpenda ombaomba amwaga unga

Weita mpenda ombaomba amwaga unga

Na DENNIS SINYO

MECHIMERU

MWANADADA aliyekuwa weita katika hoteli moja hapa alipoteza kazi yake kwa kuwa na mazoea ya kuwaomba wateja pesa.

Inasemekana mwanadada huyo alikuwa na mazoea ya kuwakimbilia wateja matajiri kuwahudumia.

Kila mara akimaliza kuwahudumia, alikuwa akiwaomba wamuachie kitu kidogo. Inasemekana wenzake walikasirishwa na tabia yake wakidai ilikuwa ikiaibisha hoteli hiyo.

Hata hivyo, demu aliwaambia wakome kumuonea wivu kwa kujua kazi.

Duru zaarifu kwamba, alikuwa akifanikiwa kwenda nyumbani na zaidi ya sh 20,000 alizopata kutoka kwa wateja matajiri kama tip.

Hii haikuwafurahisha wahudumu wenzake waliosema hakuwa na heshima.

“Badala ya kuwahudumia wateja, yeye anatumia nafasi hiyo kuwaomba pesa,’’aliteta mhudumu mwenzake. A

lipokosa kubadilisha tabia, wenzake walimripoti kwa meneja lakini akakana madai hayo na kusema walikuwa wakimuonea wivu kwa kupendwa na wateja kwa sababu ya huduma zake nzuri kwao.

Hata hivyo, kitumbua chake kiliingia mchanga wakati mteja mmoja alipoamua kulalamika kwa meneja kwamba demu alikuwa amemuomba pesa.

Yasemekana baada ya kumhudumia mteja huyo, alimuomba Sh5,000, jambo ambalo mteja huyo hakufurahia.Aliamua kumjuza meneja kuhusu tukio hilo ili hatua ichukuliwe.

Lakini alipoulizwa tena, mwanadada huyo alidai hakuwa amefanya kosa lolote. “Kwani shida iko wapi nikijitafutia hela? Huu mshahara haba haunisaidii kitu
chochote ndio maana natafuta mbinu ya kujisaidia,’’alisema mhudumu huyo.

Kulingana na mdokezi, meneja alikasirika na kumpiga kalamu. Alipokuwa akiondoka, demu aliwalaumu wenzake kwa kumuonea kijicho na kumsaliti lakini akaapa kwamba alikuwa na njia nyingi za kupata riziki na wala si hotelini pekee.

…WAZO BONZO…

 

You can share this post!

Mawimbi makali ya Jubilee, Ruto, Miguna na NASA yamgonga...

TAHARIRI: IPOA ilikosa kuafikia matarajio ya wengi

adminleo