• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Beki Mandela apata hifadhi nchini Afrika Kusini huku Kibwage akiingia katika sajili rasmi ya Sofapaka

Beki Mandela apata hifadhi nchini Afrika Kusini huku Kibwage akiingia katika sajili rasmi ya Sofapaka

Na CHRIS ADUNGO

DIFENDA wa Harambee Stars, Brian Mandela Onyango ameingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Tshakhuma Tsha Madzivhandila FC (TMM FC), ambacho awali kilijulikana kama Bidvest Wits.

Mandela ambaye ametia saini mkataba wa mwaka mmoja na TMM FC, hakuwahi kupata kikosi cha kuchezea baada ya kuagana na Maritzburg United ya Afrika Kusini kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Nyota huyo sasa amejumuishwa rasmi katika kikosi kitakachotegemewa na TMM kwenye kampeni za Ligi Kuu (PSL) muhula huu wa 2020-21.

Kutokuwepo kwa kiungo Victor Wanyama wa Montreal Impact ya Canada, kulimpa Mandela fursa ya kuvalia utepe wa unahodha wa Harambee Stars katika mchuano wa kirafiki uliowakutanisha na Chipolopolo ya Zambia uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 9.

Stars ya kocha Francis Kimanzi waliibuka na ushindi wa 2-1 katika mechi hiyo waliyoitumia kujiandalia kwa michuano miwili ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 dhidi ya Comoros mwezi Novemba.

TTM FC ina makao yake makuu katika Mkoa wa Limpopo, Afrika Kusini. Kikosi hicho kilichowahi kushiriki Ligi ya Daraja la Tatu nchini Afrika Kusini, ABC Motsepe League, kilipanda ngazi kunogesha PSL mnamo Julai 2017 baada ya kutwaa umiliki wa klabu ya Milano United FC na kuitwa Bidvest Wits.

Kwingineko, Sofapaka ambao walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2009, wamekamilisha usajili wa aliyekuwa beki matata wa KCB, Michael Kibwage kwa mkataba wa miaka miwili.

Kibwage, 23, anajiunga na ‘Batoto ba Mungu’ bila ada yoyote baada ya kandarasi yake na KCB kutamatika mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Sogora huyo alikuwa pia akiwaniwa na AFC Leopards pamoja na mabingwa watetezi na washindi mara 19 wa Ligi Kuu, Gor Mahia.

“Nafurahia kuwa hapa, katika kikosi ambacho kitanipa jukwaa mwafaka zaidi la kujikuza kitaaluma. Licha ya kuhakikishwa nafasi katika kikosi cha kwanza, nitalenga kujitahidi zaidi na kuwavunia waajiri wangu wapya mataji muhimu,” akasema Kibwage ambaye ni mwanasoka wa zamani wa FISA Academy, AFC Leopards na Kakamega Homeboyz.

Kibwage aliwahi pia kufanyiwa majaribio na vikosi viwili vya Afrika Kusini – Highlands Parks FC na TS Galaxy FC.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa Shule ya Upili ya Mukumu, anakuwa mchezaji wa nane baada ya Isaac Mitima, Michael Karamor, Michael Bodo, Kevin Omondi, Roy Okal, Lawrence Juma na Paul Kiongera kusajiliwa na Sofapaka.

You can share this post!

Babake Farida Karoney azikwa nyumbani Kamobo

Chelsea yatuma Moses kambini mwa Spartak Moscow kwa mkopo