TAHARIRI: Serikali ifafanue nani ndiye shujaa
Na MHARIRI
KWANZA, heri ya Sikukuu ya Mashujaa kutoka kwa Usimamizi wa gazeti la Taifa Leo.
Hii ni siku muhimu ambayo kabla ibadilishwe jina kutoka Kenyatta Day, ilikuwa ikitumiwa kuwakumbuka watu waliohusika na kupigania uhuru wetu. Lakini tuliporekebisha Katiba mwaka 2010, tuliweka Kifungu cha 9 (3) (b) kinachotaja kwamba sasa ni Siku ya Kitaifa ya Mashujaa na itaadhimishwa Oktoba 20 kila mwaka. Siku nyingine mbili za kitaifa ni Madaraka (Juni 1) na Jamhuri (Desemba 12).
Ingawa Katiba inatambua siku hizo tatu, maelezo ya kina hasa kuhusu Sikukuu ya Mashujaa hayapatikani kwenye katiba hiyo wala sheria zilizoundwa na Bunge kuhusiana na sikukuu za umma.
Waliotoa maoni yao mbele ya Kamati ya Profesa Yash Pal Ghai na baadaye kwa ile ya Nzamba Kitonga, hawakufafanua wanataka siku hii iwatambue mashujaa wakiwa akina nani. Inaonekana ni kama baadhi ya watu waliohisi kuwa walishiriki kupigania uhuru lakini wakasahauliwa, walitaka na wao watambuliwe.
Kwa sababu hiyo, hata walioandika Katiba hawakuwa na maelezo sahihi ya kumjua mtu anayestahili kuitwa ‘Shujaa’. Neno hili linatokana na neno la Kiarabu lenye maana ya mtu mwenye ujasiri, mtu awezaye kukabili mambo ya hatari bila hofu. Kwa maana hii, Sikukuu ya Mashujaa yafaa kuwatambua na kuwatuza watu walioonyesha ushujaa au kukabili matatizo bila ya uoga.
Lakini kwa kuwa Wakenya wengi hawajajihusisha kuelewa Kiswahili, wameishia kufasiri neno la Kiingereza ‘hero’ ambalo maana yake ni mtu anayependwa kutokana na ujasiri wake, mwenye ufanisi na sifa za kipekee.
Kutokana na kukosekana kwa maana halisi ya Mashujaa, kamati inayosimamia Sherehe za Kitaifa imekuwa ikikusanya kila mtu ambaye, machoni mwa wanasiasa, anachukuliwa kuwa shujaa. Huenda ikawa sababu miaka mitatu iliyopita, tulishuhudia watu wa kila aina wakiwemo masosholaiti na wanamuziki wakituzwa.
Serikali baada ya hapo ilimteua Tom Nyamorata kuja na kanuni na vigezo vya kuwateua mashujaa.
Serikali haijaweka hadharani mapendekezo aliyokuja nayo. Haijaeleza watu hawa wanaotuzwa leo walitambuliwa kivipi na wamekuwa na mchango upi kwa nchi yetu.
Japokuwa tungependa kufurahisha marafiki wetu wa kisiasa na kibiashara, ni muhimu kuweka wazi njia zinazotumiwa kuwateua wanaosherehekewa, ili kusiwe na maswali yasiyokuwa na majibu.