Makala

Bei ya samaki yapanda kipindi hiki cha janga la corona

October 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

WAFANYABIASHARA wanaouza samaki Nairobi wanasema wanaendelea kukadiria hasara katika uuzaji wa bidhaa hiyo.

Hii ni kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya samaki hasa baada ya mkurupuko wa virusi vya corona nchini (Covid-19) Machi 2020.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Mourine Ombiri, amesema bei ya samaki inaendelea kupanda licha ya mvua kuanza kunyesha, ambayo anasema huchangia ongezeko la samaki kwenye ziwa au bahari.

“Awali, upungufu wa samaki ulisababishwa na juakali. Bei inaendelea kupanda licha ya mvua kuanza kunyesha, tunakadiria hasara,” Mourine akasema.

Mfanyabiashara huyo wa kiungani mwa jiji la Nairobi, alisema samaki aliokuwa akinunua kati ya Sh60 – 70 kila mmoja, na kuuza Sh100, kwa sasa wanagharimu Sh80 au Sh90. “Ninapata faida ya Sh10 pekee, kwa sababu wateja wamezoea Sh100 samaki wa bei ya chini. Kuwashawishi bei imepanda si rahisi,” akaelezea.

 

Muuzaji wa samaki kiungani mwa jiji la Nairobi. Bei ya samaki imepanda kipindi hiki cha janga la Covid-19. Picha/ Sammy Waweru

Ongezeko hilo, pia limeshuhudiwa kwa samaki wa kadri na wale wakubwa.

“Samaki tuliokuwa tunauziwa Sh100 na kuuza kati ya Sh150 – 200, tunawanunua Sh150,” akasema Jecinta Anyango.

Wafanyabiashara hao wanasema hutoa samaki eneo la Nyanza. Huku bei ya mafuta ya dizeli na petroli ikiendelea kuongezeka, wanasema gharama ya kusafirisha bidhaa imekuwa ghali.

“Hapa kuna ununuzi na gharama ya kusafirisha, kimsingi tunaunda hasara badala ya kujiendeleza. Hata tukiunda faida, ni kiduchu sana,” akalalamika Jecinta.

Wafanyabiashara hao wanaiomba serikali kuweka mikakati murwa kuimarisha sekta ya ufugaji samaki na uvuvi nchini, ikiwa ni pamoja na kutathmini bei ya mafuta ili kupunguza gharama ya uchukuzi.

Samaki ni kati wanyama wanaosifiwa kuwa na nyama tamu, na iliyosheheni madini ya Protini.