• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 7:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya umilisi wa lugha ya Kiswahili katika uwanja mpana wa kiakademia

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya umilisi wa lugha ya Kiswahili katika uwanja mpana wa kiakademia

Na MARY WANGARI

KWA kawaida matumizi ya lugha ya Kiswahili hasa nchini Kenya hujitokeza katika mazingira yenye wingi-lugha kwa maana kwamba kuna lugha nyingi za kwanza zinazotumika katika jamii.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wanaojifunza lugha ya Kiswahili huwa na viwango vinavyotofautiana vya umilisi wa kiisimu katika lugha ya Kiswahili.

Hata hivyo, ni muhali kubainisha bayana viwango hivyo anuai vya kila mwanafunzi binafsi na hali hiyo ndiyo inayoathiri umilisi wa wanafunzi kuhusiana na lugha ya Kiswahili.

Tafiti za kina zinahitajika ili kukusanya data muhimu zitakazowezesha wadau wa kiakademia kubuni mitaala na mikakati muhimu ya kuimarisha ufundishaji wa kiisimu katika matumizi ya Kiswahili.

Utafiti kuhusu umilisi wa lugha pia unawezesha kutathmini iwapo nadharia ya umilisi wa inajitosheleza kiisimu katika kutafiti masuala ya ujifunzaji na ufunzaji wa isimu katika lugha ya Kiswahili.

Umilisi wa lugha una manufaa chungunzima jinsi inavyoashiriwa na wanaisimu mbalimbali ifuatavyo:

Kwa mujibu Carell (1989) anafafanua kuwa mtu anayefahamu lugha na kuwa na umilisi wa kiisimu katika lugha hiyo huonekana kuwa na ufunguo wa kufanikiwa katika masomo yake ya kiakademia.

Kwa upande wake Adams (1993) anahoji kuwa uwezo wa kusoma na kuzungumza ni stadi muhimu kwa kupata masomo ya juu ya kiakademia, ambapo stadi hizo hufuatwa na kusikiliza na kuandika.

Uandishi wa kiakademia hasa kuhusu isimu hata hivyo, ni suala la kutatanisha hasa miongoni mwa wanafunzi.

Hali hiyo hasa inachangiwa na mielekeo hasi kuhusu isimu katika lugha ya Kiswahili, jambo linaloweza kutatuliwa kupitia kuwapa motisha wanafunzi na wanajamii wanaosheheni viwango tofauti tofauti vya umilisi wa lugha.

Ni muhimu kuelewa kuwa lugha inasheheni vipengele mahsusi vinavyoashiria jinsi umilisi wa kiisimu katika lugha ya Kiswahili unavyobadilika kulingana na mtu binafsi na anakoishi.

Naye Rubin (1992) anadai kuwa ni vigumu kupima vipengele vinavyoonyesha umilisi wa kiisimu katika lugha, japo upimaji huo huegemea zaidi katika uwezo wa mzungumzaji kutumia kanuni za lugha katika ama kusoma, kuzungumza au kuandika.

Mwanaisimu Rubin anafafanua kuwa mabadiliko hujitokeza na kuonekana katika matumizi ya lugha husika, mwanafunzi anapozimudu kanuni za kisarufi katika kuzungumza na kuandika makala ya kiusomi.

[email protected]

Marejeo:

Adams, D. (1993). Defining education quality. Pittsburgh, Pennsylvania: University of Pittsburg Press

Carell, D. (1993). Metacognitive strategy training for ESL reading. New York City: Wiley Browse pub, Ltd.

You can share this post!

Kimanzi hana kazi Harambee Stars

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umuhimu wa tafiti kuhusu umilisi...