Habari Mseto

Wazee wa Kaya kujenga kituo kuenzi Mekatilili

October 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WAZEE wa Kaya wa jamii ya Mijikenda wameanza kuchangisha pesa ili kupata Sh10 milioni kununua ekari mbili za ardhi ambapo watajenga kituo cha utafiti kwa heshima ya mpiganiaji uhuru Mekatilili Menza.

Wazee hao wananuia kujenga kituo hicho eneo la Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Mwenyekiti wa Muungano wa Kitamaduni Wilaya ya Malindi (Madca) Emmanuel Mnyaya, alisema kituo hicho kitavutia watu kutoka kote ulimwenguni kujifunza kuhusu utamaduni wa jamii ya Mijikenda na jinsi Mekatilili Wa Menza alivyowaongoza kupigania uhuru.

”Kituo hiki cha kihistoria katika Shakahola ni chenye umuhimu mkubwa kwa sababu ndipo uasi dhidi ya utawala wa kikoloni ulipoanzia baada ya Mekatilili kumzaba kofi mkoloni kutoka Uingereza na hivyo kuibua uasi kote nchini,” alisema.

Mekatilili, anayefahamika pia kama Mnyazi wa Menza, alizaliwa eneo la Mtsara wa Tsatsu, Ganze mnamo 1840, na ameripotiwa kusafiri kutoka kijiji kimoja hadi kingine akikusanya jamii ya Wagiriama kupigana dhidi ya unyanyasaji uliofanyiwa watu weusi na walowezi kutoka Uingereza.

Akizungumza baada ya kukamilisha matembezi ya kilomita 68 kutoka Malindi hadi Shakahola kuhubiri amani kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa, Bw Mnyaya alisema wakazi wa eneo hilo walikuwa wameanza kuuza ardhi, jambo lililowashangaza kwa kuwa ardhi hiyo itaishia mikononi mwa wasiojua umuhimu wake.

”Gharama ya kujenga kituo hicho inaweza kufikia zaidi ya Sh10 milioni kiasi ambacho ni kikubwa, kwa sasa tunasaka Sh1milioni ili kuanza mchakato wa ununuzi na ikiwa Wakenya wataweza kuchangia tutaweza kujenga,” alisema.

Wazee hao pia walizindua nambari ya simu itakayotumika kuchangisha hela kutoka kwa wahisani wakisema kituo hicho kitawezesha vijana na hata wasomi kujifunza historia ya jadi ya Wamijikenda.

Katika hotuba yake na Mashujaa Dei akiwa Kisii, Rais Uhuru Kenyatta alimtambua Mekatili kwa ujasiri wake uliomfanya kutoroka jela alikozuiliwa na wakoloni eneo la Kisii na Kismayu, Somalia.

Kwingineko, serikali ya Kaunti ya Meru imetaja barabara mbili kwa heshima ya wapiganiaji uhuru Field Marshal Mwariama na Field Marshal Baimungi.

Hatua hiyuo imejiri baada ya bunge la kaunti hiyo kupitisha sheria inayotoa mwelekeo kuhusu wanaofaa kutambuliwa kama mashujaa katika kaunti hiyo.

Gavana Kiraitu Murungi alisema khatua hiyo itatia moyo familia zao.

“Serikali yangu pia itawalipia Bima ya Kitaifa ya Hospitali, NHIF, jamaa wa familia walio na miaka zaidi ya 75,”alisema Bw Murungi Jumatatu alipokuwa akipatia mitaa hiyo majina hayo.

Alisema wakazi watakaofanya vyema katika taaluma zao sasa watatambuliwa na kutuzwa kwa heshima ili kusherehekea ufanisi wao.

Heshima hiyo itakuwa kwa watu binafsi ambao utendakazi wao katika nyanja mbalimbali ni wa kipekee katika kuhimiza vijana pamoja na kuendeleza utamaduni.

Kamati pia imebuniwa itakayotwikwa jukumu la kuteua wafanyakazi bora watakaotuzwa.

Kamati hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Dkt Gerrishon Mwiti, tayari imeanza kuandaa orodha ya mashujaa wa Meru.

CHARLES LWANGA, MARY WANGARI NA GITONGA MARETE