Makala

GWIJI WA WIKI: Prof Kithaka Wa Mberia

October 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

WAKATI ndiyo raslimali na hazina ya pekee muhimu zaidi ambayo sisi binadamu tunayo kwa kiwango sawa.

Ukitumia hazina hii vizuri, utafaulu katika shughuli zako na utafika mbali.

Kila binadamu ana kipaji ambacho ni wajibu wake kukitambua na kupalilia. Huwezi kujiendeleza maishani iwapo hujiamini. Kujiamini ni chanzo cha ubunifu wa aina yoyote.

Kupiga hatua katika taaluma yoyote kunahitaji mtu kujiheshimu na kuongozwa na subira. Haiwezekani kabisa kwa mambo yote kuja kwa wakati mmoja. Ufanisi ni zao la bidii, nidhamu, imani na stahamala. Milango ya heri hujifungua yenyewe kwa watu wenye sifa hizi.

Chagua maono yenye matarajio, ota ndoto kubwa zenye thamani na uwe tayari kuzitolea jasho. Ndoto hukua na kunawiri iwapo itanyunyiziwa jasho! Jifunze kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo kisha teua kushindana na wakati. Thamini hicho unakichokifanya, jitume na waulize wajuao zaidi yako.

Huu ndio ushauri wa Prof Kithaka wa Mberia – mshairi, mwanaisimu, mwandishi na msomi na mtetezi wa haki ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Kithaka wa Mberia alizaliwa mnamo Agosti 8, 1955 katika kijiji cha Keraka, Kaunti ya Tharaka-Nithi.

Alianza safari yake ya masomo mnamo Mei 1963 katika Shule ya Msingi ya DEB Karethani, Tharaka alikosomea kwa miaka mitatu kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Gatunga, Marimanti, Tharaka kwa miaka minne.

Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mnamo 1969 na akapata nafasi ya kusomea katika shule maarufu ya Chuka Boys, eneo la Karingani, Tharaka-Nithi kuanzia 1970.

Baada ya kuufanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (EACE) mnamo 1973, Kithaka wa Mberia alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance, Kaunti ya Kiambu kuendeleza masomo yake ya kiwango cha ‘A-Levels’ katika mwaka wa 1974. Aliufanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Sita (KACE) mwishoni mwa 1975.

Mnamo 1976, alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya B.A katika Isimu na masuala ya Jamii, Siasa na Utawala. Alihiari kuzamia zaidi masomo ya Isimu na akapata fursa ya kufundishwa na mikota wa lugha wakiwemo Prof Mohamed Hassan Abdulaziz, Prof Karega Mutahi, Prof Mohamed Bakari, Prof Lucia Ndonga Omondi, Prof Francis Katamba (Chuo Kikuu cha Lancaster, Uingereza) na marehemu Prof Jay Kitsao.

Baada ya kufuzu mnamo 1979, Kithaka wa Mberia alianza kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi chini ya usimamizi wa Prof Karega. Alifuzu mnamo 1981 baada ya kuwasilisha Tasnifu, “The Consonants of Kitharaka” na akaanza kufundisha kozi za Fonolojia katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Baadhi ya wanafunzi wake wa kwanza ni Dkt Mungania Basilio Gichobi, Dkt Hanah Chaga Mwaliwa na Prof Kineene Wa Mutiso.

Kithaka wa Mberia alianza kusomea shahada ya uzamifu (phD) katika Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1985. Kutokana na shughuli nyingi za uandishi, alichukua kipindi kirefu cha muda kukamilisha utafiti wa nyanjani.

Ilikuwa hadi Agosti 1988 alipoanza kuandaa Tasnifu ‘Segmental Morphophonology of Kitharaka with Special Reference to the Noun” chini ya uelekezi wa Prof Karega na Prof Bakari. Aliiwasilisha mnamo 1992 na akafuzu mwaka uliofuata wa 1993.

Mbali na kuwa mtahini katika vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya Kenya, Prof Kithaka wa Mberia amewahi pia kufundisha katika Chuo Kikuu cha Virginia State, Petersburg (Amerika), Chuo Kikuu cha Warsaw (Poland) na Chuo Kikuu cha Hankuk (Korea Kusini).

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Kithaka wa Mberia tangu utotoni. Akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Pili, alitunga shairi ‘The Bell’ lililochapishwa katika Jarida la Shule ya Upili ya Chuka Boys, ‘The Voice of the Mountain’.

Aliacha kabisa kuandika alipoingia Kidato cha Tatu kwa lengo la kupata fursa ya kumakinikia masomo. Ilikuwa hadi 1982, baada ya kutunukiwa shahada ya uzamili, ambapo alirejelea uandishi wa mashairi na michezo ya kuigiza.

Baada ya kampuni ya Marimba Publishers kumfyatulia diwani ‘Mchezo wa Karata’ (1997), Kithaka wa Mberia alichapishiwa tamthilia ‘Natala’ (1997), tamthilia ‘Kifo Kisimani’ (2001), ‘Bara Jingine’ (2002), ‘Redio na Mwezi’ (2005), tamthilia ‘Maua Kwenye Jua la Asubuhi’ (2007), ‘Msimu wa Tisa’ (2007), ‘Rangi ya Anga’ (2014), ‘Doa’ (2019) na ‘Mvumo wa Helikopta’ (2020) ambayo ni diwani yake ya saba.

Sita kati ya vitabu hivyo vya Prof Kithaka wa Mberia, vimetafsiriwa hadi kwa Kiingereza: ‘A Game of Cards’ (Dkt Zaja Omboga, 2011) ‘Another Continent’ (Dkt Richard Makhanu Wafula, 2011), ‘Death at the Well’ (Khalfan Kasu na Marami V. Marami, 2011), ‘Flowers in the Morning Sun’ (Khalfan Kasu, 2011), ‘Natala’ (Khalfan Kasu, 2013) na ‘The Ninth Season’ (Zaja Omboga, 2013).

Vitabu hivi vyote ambavyo vimechapishwa na kampuni ya Marimba Publishers – iliyoanzishwa na Prof Kithaka wa Mberia mnamo 1997 – vimeidhinishwa na Taasisi ya Kenya ya Ukuzaji wa Mitaala (KICD) kutumiwa kufundishia Fasihi katika shule za upili na vyuo vya humu nchini.

Mbali na ‘Natala’ iliyotahiniwa kwa muda mrefu zaidi katika Vyuo vya Mafunzo ya Ualimu nchini Kenya (2005-2015), tamthilia nyingine ya Prof Kithaka wa Mberia iliyowahi kuteuliwa kutahiniwa katika shule za sekondari za Kenya ni ‘Kifo Kisimani’ (2005-2012).

Mbali na tamthilia zake zote tatu, mengi ya mashairi ya Prof Kithaka wa Mberia yamewahi kuigizwa jukwaani kwenye Ukumbi wa Kitaifa wa Michezo ya Kuigiza (The Kenya National Theatre). Mtaalamu huyu wa Isimu anajivunia machapisho mengi ya kitaaluma katika vitabu na majarida ya kimataifa.

HUDUMA KWA JAMII

Prof Kithaka wa Mberia amehudumu katika Bodi za Usimamizi wa shule mbalimbali katika eneo la Tharaka Kusini, ikiwemo Shule ya Upili ya ABC Nkondi Girls. Kwa sasa ni kinara katika Baraza la Uongozi la Parklands Sports Club, Nairobi.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Prof Kithaka wa Mberia ni kuendelea kuandika zaidi kazi za Isimu na Fasihi ya Kiswahili na kuhudhuria makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo makuzi ya Kiswahili.

Mbali na fahari ya kuhudhuria idadi kubwa ya michezo ya kuigiza, Prof Kithaka wa Mberia amewahi kuwa mwasilishaji na mwamuzi mkuu katika mashindano mbalimbali ya tamasha za kitaifa za muziki na drama. Anajivunia tajriba pevu kuhusu jinsi sanaa za kila sampuli zinavyozamiwa na watu wa tamaduni mbalimbali.

Zaidi ya Amerika, Korea Kusini na Poland, Prof Kithaka wa Mberia amewahi pia kuzuru mataifa ya Ujerumani, China, Tanzania, Iran, Italia na Nchi ya Milki za Kiarabu (UAE).

Kwa pamoja na mkewe Anne Mberia, wamejaliwa watoto wawili – Gacheri Mberia na Nyaga Mberia.