Shule mbili zafungwa Mombasa baada walimu kuugua corona

Na MOHAMED AHMED

WIKI moja baada ya shule kufunguliwa, visa vya maambukizi ya virusi vya corona vimeanza kuripotiwa na kutia hofu wazazi, wanafunzi na walimu.

Shule mbili za upili katika kaunti ya Mombasa zimefungwa baada ya walimu na wanafunzi kuripotiwa kuwa na virusi vya corona.

Hatua hiyo ilichukuliwa siku moja baada ya wanafunzi wawili kuthibitishwa kuwa na corona kaunti ya Nandi na Kakamega.

Shule ya Tononoka na Star of the Sea ziliamriwa kufungwa mnamo Jumatatu na kulekezwa kusalia hivyo kwa wiki mbili. Kulingana na wafanyakazi wanaofanya kazi katika shule hizo watu nane walipatikana kuwa na virusi hivyo katika shule ya sekondari ya Tononoka na visa vingine vinne kuripotiwa kutoka shule ya Star of the Sea.

Walimu walikuwa wa kwanza kupatikana kuwa na virusi hivyo ambavyo vimezidi kuongezeka hususan katika Kaunti ya Mombasa.

Ripoti za kuaminika zinaeleza kuwa baadhi ya walimu wangali wanasubiri matokeo baada ya sampuli zao kuchukuliwa na maafisa wa afya kupimwa.

“Wakati mwalimu mmoja alipopatikana kuwa ana virusi ndipo sisi wengine tuliambiwa twende kupimwa na matokeo yakaja na kuonyesha wengi wana virusi. Baadhi ya matokeo yaliingia Jumatatu na imebainika wanafunzi na walimu wote wameambukizwa,” akasema mdokezi wetu katika mojawapo ya shule hizo mbili.

Taifa Leo imebaini kuwa, mnamo Jumatatu afisa wa serikali anayehusika na masuala ya elimu eneo la Pwani alifika kwenye mojawapo ya shule hizo na kuelekeza zifungwe hadi Novemba 2.

Vile vile, kulingana na barua kutoka kwa usimamizi wa shule ya Star of the Sea ambayo ilitumwa kwa wazazi wa wanafunzi shule hiyo imefungwa ili kuruhusu upulizaji dawa.

“Hii ni kukujuza kuwa shughuli za shule zimesitishwa kwa muda kwanzia Jumatatu Oktoba 19 kuruhusu upulizaji dawa. Shule itaanza rasmi shughuli za masomo mnamo Jumatatu Novemba 2, 2020,” inasema barua hiyo.

Kufungwa kwa shule hizo kunakuja wakati viongozi katika kaunti ya Mombasa wanahimiza wakazi kuendelea kuwa waangalifu kufuatia kuongezeka kwa visa vya corona jijini humo.

Kufuatia kuongezeka kwa visa hivyo, kamishna wa kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo alisema kuwa baadhi ya hospitali sasa zimejaa.

“Kupata kitanda katika hospitali hizi kubwa ambazo tuko nazo hapa kwenye kaunti ni shida kwa sababu vitanda vimejaa pomoni. Mgonjwa lazima atafutiwe sehemu ndio aweze kuingia hospitali. Tafadhalini tuvaeni barakoa zetu kama tunavyoagizwa,” akasema Bw Kitiyo wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Mashujaa katika bustani la Mama Ngina.

Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini Kenya (CIPK) Sheikh Mohammed Khalifa alisema, kuna haja ya wakazi kuzingatia masharti ambayo yamewekwa.

Aliihimiza serikali kuweka mikakati kabambe katika shule ambazo zimefunguliwa ili kulinda watoto.

“Sisi tupo na wasiwasi na watoto wetu ambao wamerudi shule. Hivyo basi tunaomba serikali iweke mikakati ambayo itawalinda. Kama wakazi ni lazima tuendelee kujichunga,” akasema Sheikh Khalifa.

Kisa cha Nandi kiliripotiwa shule ya upili ya Kebote SDA na kisa cha Kakamega kilithibitishwa shule ya wavulana ya St Peters.