Eliud Kipchoge arefusha mkataba wake na kampuni ya Isuzu EA kwa mwaka mmoja zaidi
Na CHRIS ADUNGO
MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge, ametia saini mkataba mpya utakaomshuhudia akiendelea kuwa balozi wa mauzo wa magari, bidhaa na huduma nyinginezo za kampuni ya Isuzu East Africa kwa mwaka mmoja zaidi.
Chini ya maelewano hayo mapya, Isuzu EA itashirikiana na Wafku wa Eliud Kipchoge kuinua hali ya maisha ya wanajamii kwa kuwezesha zaidi kufikiwa kwa miradi ya elimu, ukuzaji wa talanta katika michezo na uhifadhi wa mazingira.
Kipchoge ambaye ni bingwa wa dunia, alirejea humu nchini majuzi baada ya kutokea Uholanzi alikoelekea mwishoni mwa mbio za London Marathon zilizoandaliwa mnamo Oktoba 4, 2020.
Ingawa Kipchoge hakufaulu kuhifadhi ufalme wake jijini London, amefichua mipango ya kuboresha zaidi maandalizi yake kwa minajili ya mashindano yajayo katika mbio za kilomita 42.
“Kipchoge amekuwa balozi wa kutegemewa zaidi wa magari yetu aina ya pick-ups za Isuzu D-Max. Kutokana na mafanikio yake kwenye ulingo wa riadha, amechochea watu wengi kujiamini katika chochote wanachokifanya na kufanikisha ndoto zao,” akasema Mkurugenzi Msimamizi wa Isuzu EA, Rita Kavashe.
Kwa upande wake, Kipchoge alisema: “Ukikata tamaa, basi utapoteza chote ulichokijenga kwa miaka mingi na kupoteza pia fursa maridhawa za kurejea ulingoni ukiwa na malengo mapya ya kujiboresha hata zaidi.”
“Ukifanya mazoezi zaidi, basi mwanariadha bora atarejea ulingoni ukiwa na hamu ya kusajili matokeo mazuri zaidi yatakayokusahaulisha masaibu yote ya awali na kukupa fursa ya kuwa mshindi wa kuaminika zaidi,” akaongeza.
Akiwa balozi, Kipchoge amekuwa akijivunia kutumia magari ya Isuzu D-Max pamoja na mengine mawili aliyotuzwa na Isuzu EA kwa kuibuka mshindi wa mbio za Berlin Marathon mnamo 2018 nchini Ujerumani na kukamilisha kivumbi cha INEOS Challenge 1:59 jijini Austria, Vienna chini ya kipindi cha saa mbili mnamo 2019. Kipchoge alitumia Berlin Marathon mnamo 2018 kuweka rekodi mpya ya dunia ya saa 2:01:39 kwenye mbio za kilomita 42.
“Nashukuru kampuni ya Isuzu EA kwa msaada wao ambao umepania kuniwezesha kufikia nyingi za ndoto zangu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,” akasema Kipchoge ambaye kwa sasa analenga kujenga maktaba ya Sh100 milioni katika kijiji chake cha Kapsisiywa, Kaunti ya Nandi.