• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Harambee Stars yapanda hadi nafasi ya 103 kwenye orodha ya FIFA

Harambee Stars yapanda hadi nafasi ya 103 kwenye orodha ya FIFA

Na CHRIS ADUNGO

HARAMBEE Stars wamepanda kwa nafasi tatu zaidi kutoka nambari 106 hadi 103 kwenye orodha ya viwango bora vya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Oktoba 22, 2020

Hata hivyo, timu ya taifa ya wanawake almaarufu Harambee Starlets walisalia katika nafasi yao ya awali ya 137 kimataifa baada ya kuteremka nafasi nne zaidi mnamo Septemba 2020.

Kupanda ngazi za Stars kumechangiwa na ushindi wa 2-1 waliosajili katika mchuano wa kirafiki uliowakutanisha na Chipolopolo ya Zambia mnamo Oktoba 9, 2020, uwanjani Nyayo, Nairobi.

Ni mara ya pili mfululizo kwa Stars kupanda ngazi kwenye msimamo wa FIFA baada ya kuorodheshwa wa 106 kutoka nambari 107 mnamo Septemba 17, 2020.

Kenya wamepangiwa kuvaana na viongozi wa Kundi G, Comoros kwenye mechi mbili zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) chini ya kocha mpya, Jacob ‘Ghost’ Mulee aliyerithi mikoba ambayo Francis Kimanzi alipokonywa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) mnamo Oktoba 20, 2020.

Baada ya kuvaana na Comoros jijini Nairobi mnamo Novemba 9, Stars wamepangiwa kurudiana na Wanavisiwa hao jijini Moroni mnamo Novemba 21, 2020.

Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.

“Kupanda ngazi kwa Stars ni habari njema ambazo zimetujia kwa wakati mwafaka ambapo tunajizatiti kupepetana na Comoros. Hizi ni habari ambazo naamini zitatuaminisha zaidi kadri tunavyolenga kuendeleza ubabe uliodhihirishwa na kikosi dhidi ya Zambia,” akasema Mulee.

“Stars kwa sasa wanajivunia wachezaji wa haiba kubwa ambao wana kila sababu ya kuvuna matokeo mazuri katika mechi zijazo za kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 NA Kombe la Dunia 2022 nchini Cameroon na Qatar mtawalia,” akasisitiza.

Barani Afrika, Senegal wanashikilia nafasi ya kwanza na wameorodheshwa wa 21 duniani mbele ya Tunisia (26) na Algeria (30).

Zambia wameshuka kwa nafasi moja zaidi kimataifa hadi 89. Miongoni mwa mataifa wanachama wa Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Afrika Mashariki na Kati, Uganda wanashikilia nafasi ya kwanza huku wakiorodheshwa wa 76 kimataifa.

Ubelgiji wangali kileleni mwa orodha ya FIFA duniani wakifuatwa na Ufaransa, Brazil na Uingereza.

You can share this post!

Eliud Kipchoge arefusha mkataba wake na kampuni ya Isuzu EA...

Uhuru aanza kuvumisha BBI