• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Manaibu wa magavana sasa kupata sauti BBI ikipita

Manaibu wa magavana sasa kupata sauti BBI ikipita

Na COLLINS OMULO

MANAIBU wa magavana watakuwa wenye mamlaka kinyume na sasa, ikiwa Wakenya wataipitisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Hii ni baada ya ripoti hiyo kupendekeza iwe lazima manaibu hao kupewa kazi za uwaziri na magavana.

Hili linatarajiwa kuongeza usemi wao kwenye uendeshaji wa masuala mbalimbali yanayohusu kaunti.

Katiba ya sasa haijaeleza wazi majukumu ambayo wanapaswa kutekeleza, hali ambayo ni tofauti na magavana.

Kwa mujibu wa kipengele 32 cha Sheria ya Serikali za Kaunti ya 2012, manaibu wa magavana wanapaswa kuwasaidia magavana kutekeleza majukumu yao. Hata hivyo, sheria haijafafanua kuhusu majukumu halisi wanayopaswa kutekeleza.

Sheria inaeleza tu kuwa gavana anaweza kumpa naibu wake jukumu lolote kumsaidia kama mojawapo ya wanachama wa serikali ya kaunti.

Kipengele 179 (5) cha Katiba kinaeleza kwamba naibu gavana hawezi kutekeleza majukumu ya gavana kama kumteua, kumwajiri ama kumfuta kazi afisa yeyote wa serikali ya kaunti.

Hata hivyo, ripoti inapendekeza kipengele hicho kubadilishwa, na kuifanya kuwa lazima kwa magavana kuwateua manaibu wao kuwa mawaziri.

Wakati huo huo, huenda masaibu ya kaunti kucheleweshewa pesa na Serikali Kuu yakafika mwisho, kwani ripoti inapendekeza muda maalum ambao Seneti na Bunge la Kitaifa zinapaswa kupitisha Mswada Kuhusu Ugavi wa Mapato kwa Kaunti.

Ripoti inapendekeza mswada huo kupitishwa chini ya siku 30 na mabunge hayo.

Ripoti pia inatoa nafasi kwa Msimamizi Mkuu wa Bajeti kutoa nusu ya mgao wa fedha kwa kaunti ikiwa kutaibuka mkwamo wowote kwenye upitishaji wa Mswada wa Ugavi wa Mapato.

You can share this post!

Hatima ya ziara ya Ruto kesho bado haijulikani

Nimechangia kuporomoka kwa taaluma ya Oezil – Arteta