Ngilu aitunuka sifa ripoti ya BBI
Na SAMMY WAWERU
GAVANA wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu amehimiza wananchi kuzingatia masuala aliyayataja ya muhimu yaliyomo ndani ya ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ili yaweze kuwaimarisha.
Bi Ngilu amesema kuzinduliwa kwa miradi ya maji na stima ni miongoni mwa masuala ambayo Wakenya wanapaswa kuzingatia, ili wajiimarishe kimaisha.
Gavana huyo amesema kwamba ripoti iliyoandaliwa na jopokazi la mpango huo wa maridhiano, ina mengi mazuri na ya kufaa wananchi.
“Tuzingatie yale yenye manufaa kama vile kuzinduliwa kwa miradi ya nguvu za umeme na maji, ambayo kwa njia moja ama nyingine yatasaidia kina mama na vijana,” akasema Ngilu mnamo Ijumaa.
Akipigia upatu BBI, Ngilu amehimiza Wakenya kuitumia kufanya mapendekezo ya mambo yatakayowafaa.
“Kama akina mama, tutumie fursa ya mapendekezo ya BBI kushikiniza kuwepo kwa wanawake wengi uongozini,” akasema.
Alisema mapendekezo ya ripoti ya jopokazi hilo yanaashiria kuleta usawa wa jinsia katika uongozi serikalini.
Suala la uafikiaji wa thuluthi mbili ya uongozi nchini limekuwa likizua mdahalo mkali, wanawake wakidai hawajawakilishwa ipasavyo serikalini.
Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga walipokea rasmi ripoti ya BBI mnamo Jumanne wiki hii, na inatarajiwa kuwekwa wazi Jumatatu juma lijalo.
Aidha, Rais Kenyatta na Waziri huyo Mkuu wa zamani wameanza kufanya kampeni ya kuhamasisha uungaji mkono BBI, wakihoji inalenga kuunganisha taifa ikiwa ni pamoja na kuondoa joto la kisiasa linaloshuhudiwa kila mwaka wa uchaguzi mkuu.