FUNGUKA: 'Si dume suruali, nimejipata tu…'
Na PAULINE ONGAJI
TANGU jadi, jamii imetawaliwa na dhana kwamba mwanamke ndiye anapaswa kunufaika kutokana na mwili wake.
Lakini ni dhana ambayo kila kuchao, imekuwa ikikosolewa na kupanguliwa, ambapo sasa ni kawaida kwa mwanamume kumtegemea mwanamke kifedha, huku kwa upande mwingine akimnufaisha kwa mwili wake.
Japheth ni mmojawapo ya wanaume hawa. Bwana huyu ana miaka 38 na ni mkazi wa mtaa wa Zimmerman, jijini Nairobi.
Japheth hakufika mbali kimasomo kutokana na matatizo ya kifedha, ambapo ili kuepuka uchochole kule kijijini, aliamua kuuza kipande chake cha ardhi na kuhamia jijini. Alipowasili, alinunua pikipiki na kuanzisha biashara ya bodaboda.
Kimaumbile, ameumbika na mbali na utanashati wake, kwa wanaomtambua, dume hili pia limetamba katika masuala ya mahaba. Hiyo ndio sababu inayomfanya kuwa kivutio cha wanawake wengi wanaokutana naye.
Mmoja wa wanawake ambao wamenaswa na mvuto huu ni Linah, meneja katika tawi la mojawapo ya benki nchini. Ameolewa na ni mama wa watoto wanne. Mumewe Linah anafanya kazi ng’ambo ambapo yeye huja baada ya miezi mitatu na kupumzika wiki mbili kabla ya kurejea kazini. Mumewe ni bwanyenye na hivyo kwa familia hii, pesa sio tatizo.
Linah, ametekwa sana na penzi la bwana huyu kiasi kwamba ameamua kumuinua kifedha kama mbinu ya kumnata, kama anavyosimulia Japheth hapa. “Nilikutana na Linah katika harakati zangu za kufanya kazi ya bodaboda na baada ya mazungumzo, deti kadhaa na hata kumuonjesha mahaba, mwanamke alikataa katakata kuniacha.
Sababu moja inayomfanya Linah kunikwamilia ni muda ninaochukua kumshughulikia kimahaba kwa ustadi wa kipekee, tofauti na mumewe ambaye kulingana naye, huharakisha mambo na kumuacha hoi bin taaban.
Kwa hivyo yeye huja nyumbani kwangu kila wakati. Mumewe akiwa ng’ambo, anaweza kuja angaa mara nne kwa wiki nimshughulikie.
Mumewe akiwa nchini, yeye hunifahamisha na sipaswi kumpigia simu wala kumtafuta. Ila akinihitaji huja mwenyewe. Kwa mfano, huja mchana nimshushe roho kisha anarejea kwake jioni.
Nilipomuonjesha mahaba kwa mara ya kwanza, ni kana kwamba aliingiwa na kichaa sababu alianza kujawa na wivu akihofia ushindani kutoka kwa wateja wangu wa kike.
Kwa hivyo alinishawishi kuacha kazi hiyo na kuninunulia pikipiki sita zingine ili niajiri waendeshaji huku kazi yangu sasa ikiwa ni ya umeneja.
Alinifungulia duka la bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipuri vya magari. Duka hili pia ni afisi yangu. Wakati huo nilikuwa naishi katika nyumba ndogo ya chumba kimoja, ila sasa kanikodeshea jumba lenye vyumba vitatu vya kulala. Aidha, alininunulia gari ambalo yeye hulijaza mafuta kila wiki.
Hata hivyo, sharti lake kuu ni kwamba nisiwe na mwanamke mwingine na pia hataki nioe. Ili kuhakikisha hili, sina wapenzi wa pembeni. Hata hunipigia simu za ghafla za video akitaka nimuonyeshe kila chumba kuhakikisha kuwa niko pekee yangu.”