• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
UMBEA: Mahangaiko ya nje ya ndoa hayajawahi letea mtu furaha!

UMBEA: Mahangaiko ya nje ya ndoa hayajawahi letea mtu furaha!

Na SIZARINA

WANASEMAGA hakuna mwanaume wa peke yako.

Kwamba furahi naye mnapokuwa pamoja, lakini usijihakikishie kwamba akitoka huko nje bado utakuwa uko peke yako. Sina uhakika na hili, labda akina kaka mnaweza kutuelimisha zaidi.

Kama upo kwenye changamoto ya aina hii, uelewe kwamba hali hiyo huwatokea wengi. Ndivyo maisha yalivyo. Sio rahisi kuwa kwenye furaha siku zote. Zipo nyakati ngumu na zipo pia nyakati za kufurahia maisha. Ukiwa kwenye furaha, si rahisi sana kujua kama kuna mwenzako yupo kwenye maumivu.

Tujifunze kuzitambua nyakati hizi. Tujue kwamba maisha ndivyo yalivyo. Tusilie sana hadi tukakufuru. Kikubwa ni kuamini tu, ipo siku utafurahi, haijalishi upo kwenye magumu kiasi gani.

Katika mazungumzo na akina dada kadhaa, nimekutana na kauli kwamba ndoa siku hizi imekuwa ni mazoea. Wengi wakieleza jinsi walivyojitoa kuwafurahisha waume zao lakini matokeo yake yamekuwa ni kutendwa na kusalitiwa. Wengine wakanieleza kwamba pamoja na kupika mapochopocho, kutoa mahaba ya daraja la kwanza kwa mume, ila akaishia kumfumania akifanya mapenzi na kijakazi wao. “Hivi wanaume wanataka nini?” akaniuliza dada mmoja. “Mwanaume wangu nilimpa kila kitu lakini bado alinisaliti”.

Sina jibu muafaka, lakini ninavyofahamu ni kwamba suala hili lina sura mbili. Kuna upande wa wanawake wenyewe, lakini pia upande wa wanaume husika. Tukianza na wanawake, ninyi wenyewe mnatakiwa kulikataa jambo hili katika akili zenu na kutolipigia kabisa chapuo na kulifanya kama vile kampeni yenu.

Mwanamke unachotakiwa kufanya, ni kutimiza majukumu yako kwa mwenzako ambaye tayari umejiridhisha na kuona kwamba si mtu wa kurukaruka. Si mtu mwenye tabia mfarakano. Ukifanikiwa kuwa na mwenzako, tenda yale yanayokuhusu, yale uliyo na wajibu nayo, hayo mengine yasikuumize sana kichwa.

Mwanaume anayejitambua anaweza kuwa wako pekee iwapo nawe utajitoa kutimiza majukumu yako. Kweli utamsaidia. Wewe ndiye msaidizi, kwa nini sasa uache kumsaidia? Mfanye mwanaume wako awe rafiki, umjue anapenda nini na nini hapendi. Hatakuwa na muda wa kwenda nje kama anaipata furaha nzuri kutoka kwa mtu wake. Atakuheshimu.

Lakini kwa upande wa wanaume, pia mnatakiwa kujitambua. Mwanaume ujitambue wewe ni nani na nafasi yako katika familia. Kuwa mtu ambaye unajiheshimu, ambaye unatambua kwamba unapaswa kuwa na mtu mmoja maishani, ambaye mtashiriki furaha na shida zenu. Tamaa zisizofaa wakati mwingine, ni vyema kusema na moyo wako. Jiheshimu ili pia na wewe uheshimike.

Binadamu wote tumezaliwa na kasoro. Hakuna mtimilifu. Mnapokutana wawili, mkubaliane tofauti zilizopo. Mpate suluhu na mfurahie maisha kwa pamoja. Mahangaiko ya nje ya ndoa hayajawahi kumletea mtu furaha zaidi ya sononeko la moyo.

[email protected]

You can share this post!

CHOCHEO: Kumbania unyumba ni kualika vidudumtu

Bamford afunga matatu na kusaidia Leeds United kuzamisha...