• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
El CLASICO: Real Madrid yaizidi maarifa Barcelona

El CLASICO: Real Madrid yaizidi maarifa Barcelona

Na MASHIRIKA

REAL Madrid waliwapokeza Barcelona kichapo cha 3-1 kwenye gozi la El Clasico katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Oktoba 24, 2020.

Federico Valverde aliwafungulia Real ukurasa wa mabao kunako dakika ya tano baada ya kushirikiana vilivyo na Karim Benzema. Hata hivyo, juhudi zake zilifutwa na chipukizi Ansu Fati aliyesawazishia Barcelona dakika tatu baadaye.

Fati, 17, alikamilisha kwa ustadi krosi ya Jordi Alba na kuweka rekodi ya kuwa mwanasoka wa umri mdogo zaidi kuwahi kufunga bao kwenye historia ya El Clasico.

Sergio Ramos alifungia Real bao la pili kupitia mkwaju wa penalti baada ya kuchezewa visivyo na Clement Lenglet ndani ya kijisanduku katika dakika ya 63. Goli la tatu la Real ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Zinedine Zidane, lilipachikwa wavuni na kiungo matata raia wa Croatia, Luka Modric aliyemwacha hoi kipa Marc-Andre ter Stegen mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mchuano huo uliwapa Real fursa ya kutawala gozi la El Clasico kwa mara ya 97 kwenye historia, mara moja zaidi kuliko Barcelona wanaonolewa na kocha Ronald Koeman.

Ushindi kwa Real uliwapaisha Real hadi kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 13 kutokana na mechi sita. Mabingwa hao watetezi wa La Liga sasa wanajivunia alama sita zaidi kuliko Barcelona.

Akiwa kocha, Zidane kwa sasa hajapoteza mechi yoyote kati ya sita zilizopita uwanjani Camp Nou. Ameongoza waajiri wake Real kuibuka na ushindi mara tatu na kusajili sare tatu.

Real waliingia ugani kwa minajili ya mechi hiyo ya El Clasico wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Cadiz katika gozi la La Liga wikendi iliyopita, siku chache kabla ya chombo chao kuzamishwa na Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Ni mara ya kwanza tangu 1940 katika historia ya El Clasico kwa Barcelona na Real kufunga mabao chini ya dakika nane za ufunguzi wa kipindi cha kwanza.

Isitoshe, ni mara ya kwanza kwa Real kutoshindwa kwenye michuano mitatu ya El Clasico tangu 2012-13.

You can share this post!

MPIRA WA VIKAPU: Okari Ongwae afungia Bakken Bears alama 18...

Wakatoliki wataka ufafanuzi kuhusu Papa kuunga ushoga