• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Pique ataka Barcelona wabadilishe jina la Camp Nou na kuita uwanja huo Lionel Messi Stadium

Pique ataka Barcelona wabadilishe jina la Camp Nou na kuita uwanja huo Lionel Messi Stadium

Na MASHIRIKA

GERARD Pique ametaka Barcelona kubadilisha jina la uwanja wa Camp Nou na kuuita Lionel Messi Stadium licha ya kwamba nyota huyo raia wa Argentina hahusiani vyema na baadhi ya vinara wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Nusura Barcelona wapoteze huduma za Messi mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 baada ya nahodha huyo kuwasilisha ombi la kutaka aachiliwe kuondoka uwanjani Camp Nou.

Ombi la Messi liliamsha kiu ya baadhi ya vikosi maarufu vya bara Ulaya kutaka kumsajili japo akaishia kuwa kivutio kikubwa zaidi kambini mwa Manchester City nchini Uingereza.

Hata hivyo, Messi alipiga abautani ya dakika za mwisho na kufutilia mbali mipango yake ya kuhama kwa hofu ya kuvuruga zaidi uhusiano wake na Barcelona waliomlea na kumkuza kitaaluma.

Akizungumza na gazeti la La Vanguardia nchini Uhispania, Pique ametaka Barcelona kudhihirisha ukubwa wa mapenzi na heshima yao kwa Messi kwa kumjengea mnara na kuupa uga wa sasa wa Camp Nou jina lake.

“Ningekuwa Rais wa Barcelona, ningefanya mambo kwa namna tofauti,” akatanguliza Pique kwa kufichua kwamba yeye ni miongoni mwa watu waliomshawishi Messi kusalia ugani Camp Nou licha ya fowadi huyo matata kushikilia kabisa mipango yake ya kutaka kubanduka.

“Nilimsihi Messi asalie. Japo sikuwa nikikutana naye mara kwa mara wakati huo, nilimzungumzia kwa kipindi kirefu nikamsadikisha aendelee kuwa mchezaji wa Barcelona hata kama ni kwa mwaka mmoja tu,” akaendelea.

“Nilijiuliza jinsi inavyowezekana kwa mchezaji bora zaidi katika historia, ambaye amejitolea kwa muda huu wote kuchezea Barcelona, kuamka siku moja na kutuma ujumbe wa kutaka kuondoka kwa sababu anahisi kwamba waajiri wake wamekataa kumsikiliza,” akafafanua Pique.

“Uwanja wa sasa ubadilishwe jina. La sivyo, Barcelona wajenge uga mwingine kwa heshima za Messi. Itakuwa vyema tukiwakumbuka wanasoka nguli ambao wamewahi kutuchezea badala ya kuwatupa na kupuuza kana kwamba si sehemu muhimu ya historia yetu,” akasema.

Pique, 33, hajawahi kuficha maazimio yake ya kuwa Rais wa Barcelona siku moja. Uchaguzi ujao wa Barcelona utaandaliwa mwaka ujao wa 2021 na mfanyabiashara Victor Font ndiye mwaniaji wa pekee ambaye amejitokeza kumpinga Josep Maria Bartomeu katika wadhifa wa urais wa Barcelona.

Pique amewataka pia Barcelona kuazimia haja ya kuwaajiri baadhi ya wanasoka wao wa zamani wakiwemo – Pep Guardiola, Xavi Hernandez na Carles Puyol.

Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi kambini mwa Barcelona, mnamo Julai 2020 baada ya wanachama sita wa Bodi ya Usimamizi ya kujiuzulu.

Mbali na Emili Rousaud na Enrique Tombas waliowahi kushikilia wadhifa wa urais wa Barcelona, wanachama wengine wa Bodi waliong’atuka ni wakurugenzi wanne wakiwemo Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Teixidor.

Katika barua yao ya kujiuzulu, sita hao waliangazia pia jinsi Barcelona inavyokosa mpango madhubuti wa kukabiliana na athari za kifedha zitakazotokana na virusi vya homa kali ya corona.

Katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji, Barcelona waliagana na idadi kubwa ya wanasoka wakiwemo Arthur Melo aliyetua Juventus, Ivan Rakitic aliyejiunga na Sevilla na Nelson Semedo aliyeyoyomea Wolves.

Wengine ni Arturo Vidal aliyesajiliwa na Inter Milan na Luis Suarez aliyeingia katika sajili rasmi ya Atletico Madrid.

You can share this post!

EPL: Arteta amtia nari Aubameyang afunge mabao dhidi ya...

Pigo Manchester City Aguero akirudi tena mkekani baada ya...