Habari Mseto

Waliopinga marekebisho ya katiba sasa wabadili kauli

May 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WYCLIFFE KIPSANG’

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto, ambao awali walipinga vikali wito wa kutaka kura ya maamuzi iandaliwe ili kufanyia mabadiliko Katiba, sasa wamebadili msimamo wao kwa kusema kuwa mabadiliko hayo ni muhimu kwa ustawi wa nchi.

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei (pichani) na Mbunge wa Soy, Caleb Kositany Jumatano walisema mabadiliko ya Katiba yatawezesha serikali kutimiza miradi yake ya maendeleo.

“Kuna madai kwamba baadhi yetu katika chama cha Jubilee tunaogopa kura ya maamuzi. Huo si ukweli. Kura ya maamuzi ya kubadili Katiba ifanyike sasa ndipo serikali ianze mchakato wa kutekeleza ahadi zake kuu nne za maendeleo,” akasema Bw Cherargei.

Wawili hao, hata hivyo, walishutumu kiongozi wa ODM, Raila Odinga kwa kutumia mwafaka wake wa kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta kutaka ‘kuingia’ mamlakani kwa njia ya mkato.

“Tumekuwa tukishuku mwafaka baina ya Bw Odinga na Rais Kenyatta. Mwafaka huu sasa unatumiwa na watu wachache kujinyakulia mamlaka na kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa 2022,” akasema Seneta Cherargei.

Viongozi wengine kama vile mbunge wa Turbo, Janet Sitienei, hata hivyo, walipinga wito wa kuandaa kura ya maamuzi huku wakisema kuwa kuna matatizo mengi yanayozonga nchi na yanahitaji kushughulikiwa badala ya kufanyia mabadiliko Katiba.

Akihutubia wanahabari mjini Eldoret, Bi Sitienei alisema kuwa kuna haja ya kupatia kipaumbele janga la mafuriko yanayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Fedha wanazotaka kutumia kuandaa kura za maamuzi zitumiwe kuwahudumia waathiriwa wa mafuriko na kununulia wakulima mbolea,” akasema mbunge huyo ambaye alichaguliwa kama mwaniaji huru.

Wito wa kuandaa kura za maamuzi ili kubadilisha Katiba umetishia kusambaratisha mwafaka baina ya Waziri Mkuu huyo wa zamani na Rais Kenyatta. Bw Ruto anapinga vikali pendekezo la kubadilisha Katiba ili kubuni vyeo zaidi, kikiwemo kile cha waziri mkuu.

Bw Ruto amesisitiza kuwa uamuzi wa serikali ya Jubilee kushirikiana na viongozi wa upinzani haukulenga kubuni vyeo zaidi.

Naibu wa Rais ameshikilia kuwa mwafaka baina ya Kiongozi wa Nchi na Bw Odinga unafaa kunufaisha wananchi na wala si wanasiasa wachache.

“Umoja wa kitaifa tunaopigana si wa kugawana vyeo. Hata kama tunahitaji kubadili Katiba tusibuni vyeo vipya kama vile wadhifa wa waziri mkuu,” Bw Ruto alisema alipokuwa akihutubu katika Kaunti ya Nandi mnamo Jumapili.

“Wakenya wana uwezo wa kuchagua viongozi wanaowapenda na wala si watu wachache kuketi mahali fulani wakinywa chai,” akaongezea.

Hapo Jumanne, Bw Ruto alimshambulia Bw Odinga akitaja wanaoitisha mabadiliko kama watub wazembe ambao wanatafuta kisingizio cha Katiba kila mara wanaposhindwa.