Habari Mseto

Daktari bandia Mugo wa Wairumu ahukumiwa kifungo cha miaka 11

October 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

DAKTARI bandia , James Mugo Ndichu almaarufu Mugo Wairimu almaarufu Dr Jimmy Jumatano alihukumiwa kifungo cha miaka 11 au alipe faini ya Sh1,420,000 alipokiri mashtaka ya kuendesha kliniki mtaani Kayole kinyume cha sheria , mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya Milimani, Bi Sarah Nanzushi.

Mugo, ambaye amekuwa rumande kwa muda wa miaka miwili alikiri mashtaka sita na kuomba korti imhurumie ikitilia maanani amekuwa gerezani kwa muda mrefu.

Akiwasilisha ushahidi, kiongozi wa mashtaka Bw James Machira, alisema maafisa wa polisi wa kikosi cha Flying Squad Bw John Njoroge waliarifiwa kuhusu daktari bandia aliyekuwa anatoa huduma za matibabu bila leseni.

“Inspekta Njoroge aliongoza maafisa wa polisi kutekeleza oparesheni katika eneo la Kayole kaunti ya Nairobi na kumtia nguvuni mhusika,” Bw Machira aliambia korti.

Mahakama ilifahamishwa polisi walifika katika Kliniki ya Millan Health International Limited. Bw Machira alisema polisi walikuwa wameandamana na kinara wa Bodi ya Kutoa Leseni kwa Madaktari na Wauguzi Dr Daniel Yumbya.

“Ndichu alijitambua kwa Dr Yumbya kuwa yeye ni Dr Jimmy. Aliitishwa leseni za kuendeleza huduma za upimaji na kuendeleza biashara ya matibabu. Hakuwa nazo. Pia hakuwa na leseni ya kufungua duka la kuuza dawa. Vile vile aliwekeza kwa hospitali na duka la dawa katika jengo ambalo halikuwa limeidhinishwa na Bodi ya Dawa na Sumu,” Bw Machira alimweleza hakimu.

Mshtakiwa huyo, mahakama ilifahamishwa alikuwa ameajiri wafanyakazi wawili  Victor Gathiru Kamunya na Risper Auma ambao hawakuwa wamehitimu.

Bi Nanzushi aliombwa na Bw Machira achukulie hilo kuwa kosa mbaya kwa vile wakenya wengi waliofika katika hospitali hiyo ya Mugo ambaye ni daktari feki walihatarisha maisha yao.

“Naomba hii korti imchukulie mshtakiwa hatua kali ijapokuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza. Alihatarisha maisha ya Wakenya wengi kwa kuwapa madawa ilhali alijua hakuwa hana ujuzi na hajapokea mafunzo kutoka kwa taasisi husika za serikali,” alisema Bw Machira.

Akijitetea, Mugo, aliomba msamaha na kusema amekuwa rumande miaka miwili sasa.

“Naomba korti itilie maanani kwamba nimekaa rumande kwa muda mrefu na nimeteseka mno. Sikupewa dhamana,” Bw Mugo aliomba.

Bi Nzanushi alisema makosa aliyofanya mshtakiwa hutolewa kifungo kikali. Katika mashtaka sita aliyoshtakiwa alimtoza faini ya Sh1,420,000 ama atumikie  kifungo gerezani cha miaka kumi na mmoja na miezi mitano.

Bi Nanzushi alitupilia mbali ombi la mshtakiwa la kutaka arudishiwe simu zake mbili.

Bw Machira alimweleza hakimu, Mugo anakabiliwa na kesi nyingine ya ubakaji ambapo anadaiwa aliwabaka wanawake waliofika katika kliniki yake kupokea matibabu. “Simu hizi zitatumika kama ushahidi.”