MATHEKA: Itakuwa makosa makubwa kupuuza wakosoaji wa BBI
Na BENSON MATHEKA
SIO siri kwamba joto la kisiasa litapanda nchini ikiwa mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) yatapingwa.
Kampeni za kura ya maamuzi zitakazofuatia zinaweza kuzidisha joto hili na pengine kugawanya nchi.
Migawanyiko hii inapaswa kuwa ya kimaoni, sio ya kikabila au kimaeneo. Ni hali ya kawaida katika nchi inayokumbatia demokrasia halisi kwa watu kutofautiana kwa maoni lakini wanadumisha heshima kati yao na nchi yao.
Ni makosa kwa viongozi kutumia mjadala au kampeni kuhusu ripoti hii kusuluhisha tofauti zao za kibinafsi, kisiasa au hata kibiashara.
Itakuwa makosa kwa wanasiasa kutumia kampeni hizi kuchochea jamii zao dhidi ya jamii nyingine na itakuwa makosa kwa wanasiasa kushambuliana wenyewe kwa wenyewe au jamii zao.
Ikiwa hali kama hii itazuka, lengo la BBI ambalo tumefahamishwa kuwa ni kuunganisha Wakenya, halitaafikiwa. Baadhi ya viongozi wamekuwa wakilalamika kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato huo au maoni yao hayakuzingatiwa kwenye ripoti ya mwisho.
Kwa sababu waasisi wa mpango huo walitufahamisha kuwa milango iko wazi kwa yeyote aliye na maoni ya kuboresha ripoti hiyo kuyawasilisha, kunafaa kuwa na mfumo wa kufanya hivyo.
Kwa sasa, mfumo huo haupo kwa sababu muda wa kamati iliyoandaa ripoti uliisha Juni. Hata hivyo, kutoa maoni kwa nia ya kuvuruga mchakato huo ambao bila shaka una mambo mazuri kwa nchi, hakufai kuvumiliwa.
Hapa, ningetaka kufafanua kuwa, maoni yote yanafaa kuheshimiwa, lakini vitendo vilivyo kinyume cha sheria, havifai kuvumiliwa. Hii haimaanishi wanaoikosoa wazuiwe kuandaa mikutano yao.
Kufanya hivyo ni kukaidi katiba ambayo mchakato mzima unalenga kuboresha. Muhimu ni kufanya mikutano yote ndani ya mipaka ya sheria na kuheshimu haki za wengine. Ili kuhakikisha mpango huu utaafikia malengo yake, mdahalo wa kitaifa, ulio wazi unahitajika.
Mdahalo huo ukifanyika kwa misingi ya kisheria, heshima, uadilifu, uvumilivu na nia njema, Kenya itafaidika.
Kuzima, kupuuza na kudharau maoni ya baadhi ya watu kunaweza kusababisha joto ambalo litawaacha wakiwa hawajaridhika. Inasemwa kuwa ni vigumu kuridhisha kila mtu na kwamba wengi wape.
Hata hivyo, katika masuala ya kurekebisha katiba, kauli hizi zinafaa kutumiwa katika awamu ya mwisho kwenye debe wakati wa kura ya maamuzi na sio wakati wa kampeni.
Katika kipindi hiki, kauli ya mwenye nguvu mpishe haifai kutumiwa kwa kuwa itapandisha joto la kisiasa. Uwe mdahalo wa wazi, usiogubikwa na usiri wowote. Maoni ya vijana wa mtaani yazingatiwe jinsi ya waheshimiwa yanavyozingatiwa na kila kitu kitakuwa sambamba.
Kufanya hivi kutarahisisha mchakato huu, kila Mkenya ahisi kwamba maoni yake yalithaminiwa. Makosa makubwa ambayo yanaweza kufanya BBI isitimize malengo yake ni kufumba vinywa vya wanaokosoa, kujipiga kifua kwa wanaounga na pande zote kutishiana.
Haya yakifanyika, hautakuwa wa Wakenya wote mbali utakuwa wa wanasiasa wanaotaka kutumia wananchi kutimiza maslahi yao.