• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wanyama kuwania tuzo ya Mchezaji Mpya Amerika na Canada

Wanyama kuwania tuzo ya Mchezaji Mpya Amerika na Canada

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Victor Mugubi Wanyama ametiwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo za Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) katika msimu wake wa kwanza kwenye ligi hiyo ya timu 26.

Wanyama, 29, ambaye alijiunga na Montreal Impact inayoshiriki ligi ya MLS ya ukanda wa Mashariki kutoka Tottenham Hotspur nchini Uingereza mnamo Machi 3, 2020, amechaguliwa kuwania tuzo ya mchezaji mpya wa MLS. Atawania tuzo hiyo dhidi ya wachezaji wengine 33 akiwemo mchezaji wa zamani wa Liverpool, Galatasaray na Atletico Madrid Emiliano Insua, ambaye alinyakuliwa na Los Angeles Agalaxy kutoka Stuttgart nchini Ujerumani mnamo Januari 2020.

Kiungo Wanyama, ambaye amechezea Montreal mechi nzima 20 ligini humo, pia ametiwa katika orodha ya wanaowania tuzo ya mtendaji wa wema katika jamii (MLS WORKS Humanitarian of the Year) ilio na watu wengine 25 akiwemo kipa wa zamani wa Aston Villa na Middlesbrough, Brad Guzan anayechezea Atlanta United. Tuzo ya wema katika jamii hupewa mtu aliyeng’ara uwanjani pamoja na kuchangia katika huduma za hisani. Nchini Kenya, Wanyama pia ana wakfu unaolipia wanafunzi kadhaa karo ya shule na pia imesambaza vyakula, barakoa na viyeuzi wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Wanyama na klabu yake ya Montreal wamekuwa mstari wa mbele kupinga visa vya mauaji ya watu weusi yaliyofanywa na polisi. Timu ya Montreal imekuwa ikivalia tishati zilizoandikwa maneno “Black Lives Matter” kupitisha ujumbe kuwa hata maisha ya watu weusi ni muhimu na hawafai kuuliwa kiholela.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya pia amechezea Montreal mchuano mmoja kwenye Klabu Bingwa ya Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF).

Kupitia tovuti ya MLS, MLS ilitangaza Oktoba 28 kuwa ukipigaji wa kura wa tuzo hizo utaanza Oktoba 29 na kukamilika Novemba 9. Orodha ya wanafainali wa tuzo hiyo itatangazwa Novemba 11.

“Majina ya waliochaguliwa kuwania tuzo yaliwasilishwa na klabu zao. Tuzo zenyewe zitaamuliwa kupitia kupigiwa kura na makundi matatu ambayo ni; wachezaji kutoka MLS, klabu za MLS (makocha, wakurugenzi wa kiufundi/meneja makuu) na wanahabari kutoka mashirika ya habari ya maeneo timu zao zinatoka pamoja na ya kitaifa ambayo yamekuwa yakiripoti habari za MLS katika msimu wa kawaida wa 2020,” MLS ilisema jinsi inavyopata majina ya wawaniaji.

Vitengo vingine vitakavyowaniwa ni tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka 2020 inayofahamika kama Landon Donovan, Mchezaji Bora wa mwaka chipukizi, Kipa Bora wa mwaka, Beki Bora wa mwaka, Mchezaji aliyerejea kwa kishindo baada ya kuwa nje, na Kocha Bora wa mwaka.

MLS pia imesema itatuza goli safi la mwaka pamoja na shuti hatari lililopanguliwa. Vitengo hivi viwili vitapigiwa kura kutoka Novemba 12-18 katika tovuti ya MLS.

Mbali na Wanyama, ambaye gazeti la The Athletic linadai kuwa anapokea mshahara wa Sh326.5 milioni kila mwaka, Montreal Impact pia imewasilisha majina ya mshambuliaji wa Honduras Romell Quioto kuwania tuzo ya Landon Donovan, Muingereza Luis Binks (Mchezaji Bora Chipukizi na Beki Bora) na raia wa Senegal Clement Diop (Kipa Bora). Mfaransa Thierry Henry anawania tuzo ya Kocha Bora wa mwaka.

Montreal inashikilia nafasi ya tisa kwenye ukanda wa Mashariki kwa alama 23 kutokana na mechi 21 baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Nashville hapo Oktoba 28. Timu hiyo ya Montreal inakabiliwa na hatari ya kukosa awamu ya muondoano ya ligi hiyo baada ya kichapo hicho. Inawania tiketi mbili zilizosalia dhidi ya Inter Miami, Chicago Fire na DC United (zote zimezoa alama 21), Atlanta United (19) na Cincinnati (16) zinazokamata nafasi tano za mwisho, mtawalia.

You can share this post!

AWINO: Magavana waache unafiki katika sheria mpya ya kilimo

Olunga, Wanyama wapongeza Mandela kujiunga na Mamelodi...