Wakenya wapepeta moto wa corona
Na WAANDISHI WETU
MAAMBUKIZI ya virusi vya corona yamefikia hatua ya kutisha nchini huku vitanda vikikaribia kuisha katika hospitali nyingi, na ofisi za umma na makampuni zikianza kuwatuma tena wafanyikazi nyumbani.
Maambukizi hayo yalianza kuongezeka kwa kasi tangu Rais Uhuru Kenyatta alipolegeza masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo, ambapo wanasiasa walichukua fursa hiyo kuandaa mikutano mikubwa ya hadhara isiyozingatia kanuni za Wizara ya Afya (MoH).
Katika mikutano yao, wengi wa wanaohudhuria mikutano ya viongozi hao wakiwemo Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka huwa wamesongamana na hawavai barakoa.
Jana Rais Kenyatta aliitisha Kongamano maalum hJumatano ijayo kujadili ongezeko la maambukizi. Ujumbe kutoka Ikulu ulisema kongamano hilo litajadili masuala kadhaa zikiwemo kanuni za kuzuia maambukizi na matokeo ya kuzilegeza.
“Rais amewahimiza Wakenya kuendelea kuzingatia kanuni za kuvaa barakoa wakiwa katika maeneo ya umma, kuosha mikono na kuepuka misongamano,” ukasema ujumbe wa Ikulu.
Ujumbe huo wa Rais Kenyatta ni kinaya kwani yeye mwenyewe amekuwa akihutubia mikutano yenye misongamano ya watu ambao wengi huwa hawajavaa barakoa.
Raia nao wamewaiga viongozi katika kukiuka kanuni kufuatia kufunguliwa kwa baa, maeneo ya burudani, kupunguzwa kwa muda wa kafyu na watu kuruhusiwa kukusanyika kwenye harusi, maeneo ya ibada na mazishini.
Ingawa baa zinafaa kufungwa saa nne usiku, nyingi zimekuwa zikihudumu hadi usiku wa manane na zingine hadi chee.
Hospitali nyingi zimeripoti kuwa wadi zilizotengewa wagonjwa wa corona zimejaa huku kiwango cha maambukizi kikifikia asilimia 20.5 mnamo Jumanne. Kabla ya masharti kulegezwa Septemba, kiwango cha juu cha maambukizi kilichokuwa kimerekodiwa nchini kilikuwa asilimia 13.1.
Katika jiji kuu la Nairobi, vitanda vya wagonjwa mahututi (ICU) viko karibu kujaa katika hospitali za umma na kibinafsi.
Kulingana na Baraza la Wahudumu wa Afya (KPMDUC), kuna hospitali 273 nchini zenye vitanda 7,612 vya wagonjwa wa maradhi ya kuambukiza. Kati ya hizi kuna vitanda 319 pekee vya ICU vinavyoweza kuhudumia wagonjwa wa corona.
Kaunti zinaripoti kuwa hospitali zimelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wa corona na mnamo Jumanne hospitali ya Aga Khan Nairobi ililazimika kutumia uwanja wa wazi kama wadi kutokana na idadi kubwa ya waliohitaji matibabu maalum.
“Jijini Nairobi, vitanda vya ICU vinaelekea kujaa. KNH tumebakisha vichache lakini hospitali za kibinafsi zimejaa. Kuna hatari ya janga kubwa la kiafya,” akasema Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Kuambukiza katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Dkt Loice Ombajo.
“Covid-19 sio ugonjwa wa kulaza mtu siku moja hospitalini, na hii inamaanisha ni wachache tu wanaolazwa. Hatua za dharura zinahitajika kabla ya hali kuwa mbaya zaidi,” akasema.
Kuna visa 51,851 vilivyothibitishwa nchini tangu Machi. Idadi ya vifo pia imeongezeka katika siku chache zilizopita hadi 950.
Viwango vya maambukizi vimepanda katika kaunti za mashambani na virusi hivyo vimeripotiwa pia katika taasisi za elimu.
Katika Kaunti ya Mombasa ambako visa vya maambukizi vilikuwa vimepungua pakubwa kufikia Septemba, mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Tononoka alifariki baada ya kuugua corona, siku mbili baada ya shule hiyo kufungwa walimu kadhaa walipothibitshwa kuwa na virusi hivyo.
Mwalimu mwingine wa shule ya upili ya Olmarai, eneo la Mogotio, Kaunti ya Baringo naye ameaga dunia, Mkurugenzi wa TSC katika kaunti hiyo James Nyakweba amethibitisha.
Mwenyekiti wa chama cha walimu cha Kuppet tawi la Baringo, David Toroitich alisema hali ya Covid-19 nchini inatia wasiwasi na kuitaka serikali ifikirie kufunga shule badala ya kuwahatarisha wanafunzi na walimu.
Lakini licha ya visa vya corona kuripotiwa katika shule nyingi, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha anashikilia kuwa hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.
Bunge la Kaunti ya Mombasa nalo limesimamisha vikao kwa wiki mbili baada ya madiwani wanne na wafanyakazi watatu kuthibitishwa kuwa na corona.
Katika Kaunti ya Kilifi, ofisi za serikali ya kaunti zilifungwa jana kwa siku 14 baada ya wafanyikazi 24 kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona.
Katika Kaunti ya Vihiga, ofisi za idara ya afya zimefungwa baada ya maafisa 13 kuugua.
Huko Machakos, wafanyakazi wameagizwa kufika ofisini kwa zamu ili kupunguza hatari ya kuambukizana corona.
Pokot Magharibi, huduma za matibabu na upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Kapenguria zimesimamishwa kwa muda wa siku 14 kutokana na ongezeko la visa vya Covid 19.
Mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, waumini wameingiwa na wasiwasi baada ya wahubiri kadhaa kuambukizwa na baadhi kufariki.
Ripoti ya Benson Matheka, PSCU, Collin Omulo, Nasibo Kabale, Maureen Ongala, Titus Ominde, Oscar Kakai Na Florah Koech