Makala

Mchoraji kwa zaidi ya miaka 30, ubunifu wa kipekee umempa riziki ya maana

October 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DIANA MUTHEU

“Nikiwa darasa la kwanza, mimi ndiye nilikuwa mchoraji bora wa magari shuleni kwetu,” George Karanja Mwenja, 56, ambaye kwa zaidi ya miaka 25 amekuwa akijichumia riziki kutokana na talanta yake ya uchoraji, alieleza Taifa Leo Dijitali tulipomtembelea katika kibanda chake kwa jina ‘Culture Studios International’ .

Msanii huyu ambaye ni maarufu kama ‘Ras’ miongoni mwa watu wanaomfahamu amewekeza karibu na lango la ngome ya Fort Jesus, Kaunti ya Mombasa ambapo anauza bidhaa za uchoraji.

Kinachovutia sana kuhusu kazi yake ni kuwa anatengeneza bidhaa nzuri nzuri akitumia vitu ambavyo watu hawazihitaji tena, kama vile plastiki kutoka kwa friji zilizoharibika na vifuniko vya vyupa vya soda.

Katika kibanda chake ambacho amekijenga kwa ustadi kutumia mbao kuukuu na plastiki ambazo ndizo paa na akapanda maua ambayo yamezifunika na kutengeneza kivuli kizuri, chini yake ameweka meza yake ya kazi na viti viwili.

Miongoni mwa bidhaa zilizonivutia ni vidude vyenye sumaki ambavyo mtu anaweza kuviweka mbele na kando ya friji yake kama mapambo, feni za plastiki zenye maumbo ya wanyama tofauti na gari zilizotengenezwa kutumia vifuniko vya soda.

Pia, anauza mapambo ya nyumba kutumia plastiki hizo ambazo mtu anaweza kuzianika mlangoni au ukutani, vyungu vya kupanda maua, na zaidi kibandani kwake kuna michoro iliyochorwa kwa ustadi katika vifaa tofauti kama vile karatasi, mbao na hata vitambaa.

Kuna michoro ya kawaida na pia kuna zile ambazo zinaelezea historia ya eneo la Old Town.

“Ukiwa msanii lazima uwe mbunifu. Katika kazi yangu, vitu ambavyo watu wengine hawavioni kuwa vya maana, ndivyo navitumia kutengeneza bidhaa za kuvutia, na kuziuza,” akasema Karanja huku akielezea kuwa huwa pia anachora maneno katika vibao vya kumwelekeza mtu au zinazotumika katika maduka tofauti ya kibiashara kuelezea wateja ni huduma gani zinatolewa mle.

Bidhaa zake zinauzwa kuanzia Sh200 hadi zaidi ya Sh100,000.

Karanja anasema kuwa alianza kuuza michoro hiyo katika kaunti ya Lamu kwa miaka 21, na akahamia mjini Mombasa ambapo ameuza bidhaa hizo kwa miaka minane sasa.

Licha ya kujivunia biashara yake, anasema kuwa imekumbwa na changamoto ambazo zilikuwa na uzito mkubwa sana.

Anasema mavamizi ya mara kwa mara ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab miaka ya nyuma, yalitikisa biashara yake pakubwa ndipo akahamia Mombasa.

“Biashara iliharibiwa na mavamizi ya mara kwa mara manake watalii walisusia kuja nchini na hoteli zilifungwa,” akasema huku akiongeza kuwa ghasia baada ya uchaguzi na vita vya kikabila pia vilichangia kuwepo kwa mazingira mabaya ya kufanyia kazi zake.

Kwa sasa anasema kuwa watalii wa humu nchini ndio wateja wake wakubwa kwa sababu idadi ya watalii kutoka nje imekuwa ikipungua kila mwaka, na zaidi mwaka huu, janga la corona limevuruga kila kitu.

Mwanabiashara huyo anasema kuwa rasilimali anazotumia kutengeneza bidhaa zake anazipata kutoka kwa rehani na zaidi anashirikiana na watu wa mikokoteni wanaookota taka za aina yote mitaani, ili wamkusanyie vitu hivyo na pia wamsafirishie.

“Friji zilizoharibika huwa kipato kwa watu katika sekta ya Juakali, lakini wakitoa mabati wanazozitumia, plastiki zote hutupwa ovyo. Watu wa kuokota taka wakitumia mikokoteni huziokota na kuniletea,” akasema huku akieleza kuwa anajiuza katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Whatsapp.

Karanja anasema kuwa anafurahi kuwafunza watu 20 ambao walikuwa na hamu ya kujua kuchora, na tayari wengi wameweza kujianzishia biashara zao wenyewe.

“Pia nimewafunza wanafunzi kutoka shule kadhaa za Lamu, pamoja na watoto ambao wazazi wao walihitaji niwape mafunzo nyumbani kwao,” akasema mwanabiashara huyo.

Ana matumaini kuwa watalii wa humu nchini watamiminika Pwani na kuinua biashara za wasanii wa aina mbalimbali, ambao wanauza sanaa za thamani.

Akiwa ameifanya kazi ya kuchora na pia kuongezea mvuto vifaa vya plastiki, Karanja ni mwingi wa mawaidha haswa kwa vijana, na mtu yeyote yule ambaye angependa kujichumia riziki kutumia talanta au sanaa ya uchoraji.

“Watie bidii na wasivunjike moyo manake uchoraji unalipa ukitengeneza bidhaa nzuri. Mchoro mzuri ni ule ambao mchoraji amechukua muda kuuandaa. Pia, kama unapenda kuchora, siri ni kuendelea kuchora tu,” akasema Karanja huku akiiomba serikali kuregesha masomo ya sanaa ili walimu na wazazi waweze kutambua na kukuza talanta za wanafunzi mapema.

“Masomo haya yatawasaidia wanafunzi kuwa na jambo la kufanya hata wakiwa nyumbani kwa ajili ya likizo au janga la corona, na itawaepusha kujiunga na makundi ya uhalifu ama kutumia dawa za kulevya, manake wantatumia muda huo kurembesha nchi yetu kwa michoro mizuri mizuri,” akasema Karanja.

Pia, aliwaomba wasanii wa kuchora wawe wabunifu wa kutumia bidhaa ambazo zinapatikana kwa urahisi ili kusaidia katika kusafisha mazingira, na pia kuvumbua aina mpya za michoro.

“Zaidi, talanta ya uchoraji ikikuzwa vizuri, vijana wengi wanaweza kujianzishia biashara zao wenyewe badala ya kungoja kuajiriwa,” akasema.