• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MUTUA: Iwe ni Trump au Biden, watakusaidia nini vile?

MUTUA: Iwe ni Trump au Biden, watakusaidia nini vile?

Na DOUGLAS MUTUA

NIMEWAONA Wakenya na kiherehere chao wakimtakia ushindi Rais Donald Trump wa Marekani katika uchaguzi utakaofanyika Jumanne.

Si neno, kila mtu duniani ana uhuru wa kumuunga mkono anayemtaka. Hayo ndiyo manufaa ya demokrasia; hata mke wako akiamua kumchagua usiyemtaka huna la kufanya.

Hata hivyo, Wakenya waliomtakia ushindi Bw Trump – ambaye anashindana na Bw Joe Biden wa chama cha Democrat – wanaishi Kenya, hivyo hawatapiga kura Marekani.

Ni matamanio yao kwamba Trump, sogora wa siasa kwenye chama cha Republican, ataibuka mshindi ili azuie sera mbovu za Democrats kama vile uavyaji mimba.

Pia wanamwombea sana ushindi ili azuie utekelezaji wa sera mbovu ya chama cha Democrat: uhusiano wa kimapenzi kati ya watu wa jinsia moja.Hayo ni mambo mawili makuu ambayo Mkenya na kiherehere chake, akiwa kijijini Kathonzweni, Karatina au Mbita, anatamani sana Bw Trump amtimizie.

Mara hii kiherehere hatamki hadharani, kama alivyofanya wakati wa uchaguzi wa Marekani mnamo 2016, kwamba Trump ashinde awarudishe nyumbani Wakenya wanaoishi Marekani.

Labda kiherehere ameshajua kwamba hilo si jambo rahisi hivyo kwa sababu imemchukua yapata miaka minne hivi na ombi hilo halijajibiwa.

Unajipata katika hali kinzani ukiwa ughaibuni unapoombwa msaada wa kifedha – mchango wa skuli au msiba – kutoka kwa mtu anayesema wazi mitandaoni unapaswa kurudishwa Kenya!

Hapo ndipo unapomwomba Mungu subira na hekima ili akuwezeshe kukomaa kuliko baadhi ya watu, utoe zaka tu japo shingo upande kwa kuwa nayo ni ada kwa Mungu.

Je, kwa nini Trump badala ya Biden? Kisa na maana ni kwamba Mkenya ni mcha Mungu sana na anamwona Trump kama mkristo mwenzake anayetekeleza mapenzi ya Mungu duniani.

Kwa maoni ya Mkenya niliyekwisha kusawiria, taifa tajiri na lenye nguvu zaidi duniani kama Marekani halipaswi kuongozwa na kafiri kama Biden.

Maoni ya kupendeza yakisikika, ila ni mazao ya mawazo finyu.Nimeandika na kurudia kwamba Mkenya ana kiherehere kwa kuwa ana mambo kibao tu anayopaswa kuwa akishughulikia, lakini anapata muda wa kuwaza na kuomba kuhusu yasiyomhusu ndewe wala sikio.

Sikwambii yanafanyika maelfu na maelfu ya kilomita kutoka kijijini kwake, lakini yanamkosesha usingizi.Mathalan anapaswa kuwa shughulini kutafuta ada za shule za watoto wake kwa kuwa alishatafuna pesa alizohifadhi karo akidhani shule hazitafungunguliwa mwaka huu.

Vilevile, ripoti ya jopo la maridhiano, almaarufu BBI, imetolewa hivi majuzi tu na Mkenya hajaisoma akamaliza, lakini ya nchi za watu yanamzuga sana asishughulikie ya kwake.

Kuhusu uavyaji mimba na ngono ya jinsia moja, mambo ambayo Mkenya anataka Trump akomeshe, huko nakuita kujitiatia kwenye mambo asiyoyaelewa.Hata hivyo, namwelewa Mkenya.

Ukiwa nje ya Marekani ni rahisi kutaka kunasibishwa na chama cha Republican; sera zake zinakubaliana na baadhi ya mila na desturi zetu. Lakini ukifika Marekani kwenyewe unatambua kwamba kuna mambo mengine muhimu zaidi kwako wewe binafsi kuwa hai kuliko kuzugwa akili na mimba yasiyo yako na kuchungulia vyumba vya watu vya kulala.

Chuki iliyojikita kwenye ubaguzi wa rangi ambao ni mtindo wa chama cha Republican inakujulisha kuwa wewe humo miongoni mwa watu wa kutambuliwa.Hali ni ya ‘kaa kando tutakuita tukimaliza tukujulishe tulivyokuamulia’.

Na ikiwa una haraka sana, rudi kwenu ulikotoka! Kinatambua ukristo pekee, nyingine si dini za Mungu eti.Wakati uo huo, chama cha Democrat kinamkumbatia kila mtu bila kujali rangi wala asili yake.

Kinakupa fursa ya kuketi kwenye meza ya majadiliano na kushiriki kikamilifu katika maamuzi kukuhusu wewe mwenyewe. Binadamu ana hulka ya kupenda kutambuliwa.Ukiona Mkenya anayeishi Marekani akimfanyia kampeni Bw Biden au kushiriki maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi, sasa utamwelewa. Kaida ya maumbile ni kujisitiri binafsi kwanza.

[email protected]

You can share this post!

‘Wanahabari 400 wamepoteza ajira sababu ya...

Ruto aitetea IEBC