Habari Mseto

Naibu Gavana akejeli wanasiasa wanaolipa vijana kuvuruga mikutano ya kisiasa Nyeri

October 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Naibu Gavana wa Nyeri Caroline Karugu amelaani vikali fujo zilizozuka mjini Nyeri Ijumaa kufuatia ziara ya Naibu wa Rais Willliam Ruto eneo hilo, akikejeli mtindo wa baadhi ya wanasiasa kuwalipa vijana ili kuvuruga mikutano.

Kundi la vijana wanaohusishwa na baadhi ya wabunge eneo hilo lilitishia kusambaratatisha mkutano wa Dkt Ruto, hali ambayo ilialika mzozano kati ya kundi hilo na linaloegemea upande wa Naibu Rais.

Naibu Gavana Nyeri, Bi Karugu ametaja tukio hilo kama siasa za “kitoto”, hasa Nyeri inapopokea wageni wanaotofautiana kimawazo na baadhi ya viongozi wa kisiasa eneo hilo.

“Hali ya taharuki na siasa za kitoto zimeanza kushuhudiwa Mjini Nyeri tunapopokea viongozi wenye mtazamo tofauti kimawazo,” Karugu amesema.

“Awali, ilikuwa Kalonzo (Kiongozi wa Wiper – Kalonzo Musyoka) na sasa imekuwa Ruto. Inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa kisiasa Nyeri ndio wanachochea matukio ya aina hiyo,” akaeleza.

Kulingana na Naibu Gavana huyo, Mji wa Nyeri “ni makao ya maelfu ya waheshimiwa na hauna nafasi ya viongozi wahuni na wafuasi wao wanaolipwa”.

Bi Karugu amefafanua kwamba Nyeri si ya mtu binafsi, na kwa viongozi wanaochochea fujo za kisiasa zilizoshuhudiwa wakati wa ziara ya Naibu Rais, Ruto na kiongozi wa chama cha Wiper hapo awali, iwapo hawakuhusika kuwaalika wanapaswa kusalia nyumbani.

“Ikiwa hukuwaalika na huhisi kuwalaki, kaa nyumbani. Isitoshe, inapendekezwa kipindi hiki cha virusi vya corona  (Covid-19) usalie nyumbani,” Karugu akasema.

Salamu za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga maarufu kama Handisheki na kuzinduliwa kwa Mpango wa Maridhiano (BBI), kulichangia mgawanyiko katika chama tawala cha Jubilee.

Aidha, makundi mawili, ‘Kieleweke’ linaloegemea upande wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, na ‘Tangatanga’ upande wa Dkt Ruto yaliibuka, la Naibu Rais likihisi Handisheki na BBI inalenga kuzima ndoto zake kuingia Ikulu 2022.

Katika ziara ya Ruto Mjini Nyeri Ijumaa, halaiki ya watu waliojitokeza kuhudhuria mkutano wake, walionekana kukataa kuzungumziwa na mmoja wa wabunge eneo hilo.