• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Upinzani wadai wafuasi 30 walionaswa wametoweka

Upinzani wadai wafuasi 30 walionaswa wametoweka

Na THE CITIZEN

DAR ES SALAAM, Tanzania

VYAMA vikuu vya upinzani Tanzania vimedai kuwa viongozi na wafuasi wao 30 waliokamatwa na polisi hawajulikani waliko.

Kulingana na vyama hivyo Chadema na ACT-Wazalendo, zimepita siku tatu tangu kuripotiwa kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui na bado haijulikani alipo na hali ya afya yake ilivyo.

Akizungumza na The Citizen, Katibu wa Uhusiano wa Umma wa ACT-Wazalendo, Salum Bimani, alisema pia wanawatafuta wanachama wengine 30 ambao waliripotiwa kukamatwa na vikosi vya usalama.

“Hatujamuona au kusikia kutoka kwa Mazrui tangu alipokamatwa siku tatu zilizopita. Pia, tunawatafuta wanachama wengine 30. Hatujui waliko. Tumetembelea karibu vituo vyote vya polisi, na wanaendelea kutupa jibu moja wakisema kuwa: hawapo hapa,” alisema.

Alisema chama hicho kinatoa wito kwa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, hasa Muungano wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN), na watetezi wengine ili waingilie kati na kushinikiza serikali ya Tanzania dhidi ya kuwashika na kuwafungia wanachama wake kinyume cha sheria wakati wa uchaguzi.

Bimani alisema kumekuwa na unyanyasaji wa hali ya juu wa haki za binadamu eneo hilo.

“Wanachama wengine ambao walikamatwa na polisi wamefanyiwa ukatili usioweza kutajika.”

Kulingana na Bimani, afisa mmoja mkuu wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa Ladhu ambaye alizuiliwa Jumatano, na maafisa wa usalama alipojaribu kwenda kushuhudia kuhesabiwa kura, amelazwa hospitalini baada ya kupata majeraha ikiwa ni pamoja na kuvunjika miguu na mikono.

Kupitia taarifa katika akaunti yake ya Twitter, chama cha ACT-Wazalendo kilichapisha picha za Jussa akiwa amelazwa kwenye kitanda cha hospitali akionekana kuwa na majeraha.

“Hivi ndivyo @IsmailJussa alipigwa na vikosi vya usalama jana. Huu sio ubinadamu na hali kama hii haiwezi kukubalika kwa wale wanaopenda ubinadamu. Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kutazama na kuchukulia hatua utawala wa Magufuli, ” kiliandika chama hicho kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Siku ya Ijumaa, mgombea urais wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Seif Shariff Hamad alijiwasilisha katika kituo cha polisi kama alivyoagizwa.

“Amefika katika kituo cha polisi, na tunavyoongea sasa hivi, bado yuko hapo,” Bimani alisema wakati huo.

Hamad na Prof Omar Fakih walikamatwa na polisi mnamo Alhamisi asubuhi mara tu baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari huko Zanzibar.

Kukamatwa kwao kulijiri baada ya matokeo ya awali ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuonyesha kwamba mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi, ndiye alikuwa akiongoza kwa kura nyingi.

Maafisa hao wa polisi hawakutoa maelezo kamili ya kukamatwa kwao.

You can share this post!

Walimu wataka shule zifungwe Covid ikisambaa

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ubantu na Uarabu wa Vivumishi...