• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ubantu na Uarabu wa Vivumishi vya idadi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ubantu na Uarabu wa Vivumishi vya idadi

Na CHRIS ADUNGO

INGAWA nadharia pekee inayosomeshwa vyuoni ni kwamba Kiswahili ni Kibantu kwa asili na kwa dhati yake, bado kuna hoja inayosema kwamba asili ya lugha hii ya upwa wa Afrika Mashariki ni mchanganyiko.

Mchanganyiko kwa sababu kunazo nadharia kadhaa zinazotetea chimbuko na asili ya Kiswahili kama lugha chotara au iliyotokana na Kiarabu.

Kiswahili ni lugha chotara kwa sababu kimeiga baadhi ya maneno kutokana na lugha nyinginezo kama vile Kiingereza, Kireno, Kijerumani, Kiajemi, nk. Baadhi ya watetezi wa asili ya lugha hii wanaihusisha na Kiarabu kwa kuwa mwingi wa msamiati wake umetokana nacho. Ingawa hivyo, nadharia iliyo na mashiko zaidi ni ile inayofafanua Kiswahili kama mojawapo ya lugha za Kibantu.

Sifa

Kunazo sifa mbalimbali zinazoonyeshwa na Kiswahili na kushadidia ithibati ya kwamba ni lugha yenye asili ya Kibantu. Pamoja na sifa hizo ni ushabihiano mkubwa katika matamshi ya maneno yanayorejelea maumbile asilia kama vile milima, mawe, maji, mito, misitu n.k.

Sifa nyingine inayokihusisha Kiswahili na Kibantu ni vingi vya vitenzi kuishia kwa sauti ya irabu /-a/ na uwezekano mkubwa wa vitenzi hivyo kunyambuliwa katika kauli mbalimbali.

Mwingiliano

Hata hivyo, mwingiliano mkubwa zaidi unashuhudiwa katika ngazi ya nomino ambapo majina mengi yanawezekana kupangwa katika makundi mbalimbali (ngeli) kwa kutegemea sifa za kimsingi katika umoja na wingi wa kipatanishi cha kisarufi katika kitenzi kwenye sentensi.

Kiswahili kinaonyesha mwingiliano mkubwa wa kisifa katika majina ya sehemu za mwili na hesabu ya vivumishi bayana vya idadi. Vivumishi vya idadi hugawika kuwili – vya jumla (-chache, -ingi) na bayana (-moja, -pili, -tatu, -nne, -tano, sita, saba, -nane, tisa, kumi).

Kivumishi ni neno linaloelezea ‘uvumi’ fulani kuhusiana na jina. Aghalabu katika sentensi, vivumishi hutoa habari, taarifa au maelezo zaidi kuhusu nomino. Kuna vivumishi vya aina nyingi, ikiwa tunakusudia kuvigawa katika makundi. Kunavyo vivumishi vya nomino, sifa, vimilikishi, idadi, pekee, viashiria au vionyeshi, visisitizi, virejeshi, ‘-a’ unganifu, n.k.

Katika makala haya, nitalenga kuzungumzia aina mbili kati ya hizo – vivumishi vya idadi na vya sifa. Katika aina zote mbili, kuna kanuni moja inayotawala matumizi sahihi kwa mujibu wa kanuni za sarufi.

Nayo ni kuwa vile vivumishi vyote vyenye asili ya lugha za Kibantu vinachukua viambishi awali vya jina linalokielezea, ambapo vile vyote ambavyo vina asili ya lugha za Kiarabu au nyingine ya kigeni, havibebi viambishi hivyo.

Kanuni

Kiambishi ni kipande cha neno (aghalabu silabi) kinachoweza kuambatishwa kwenye mzizi wa neno na kuunda neno jipya (Kamusi ya Kiswahili Sanifu -2013). Hivyo, kuambisha ni zoezi la kuambatanisha mofimu kwenye mzizi wa neno ili kuwakilisha hali au dhana fulani.

Kukiukwa kwa kanuni hizi hata hivyo kunaweza kuivuruga sarufi ya lugha ambayo yatupasa kuishabikia na kuitukuza (kwa usahihi) katika mawasiliano yetu ya kila siku kwa kuwa mawasiliano ndiyo dhima kuu inayotekelezwa na lugha.

Katika vivumishi vya idadi, nambari zinazochukua viambishi vya majina ni zile za Kibantu pekee. Kwa mfano; moja, mbili, tatu, nne, tano, na nane; na wala si sufuri, sita, saba na tisa.

Kwa mfano, tunasema:

(a) Wanafunzi wanane wameingia darasani.

(b) Vitabu sita vimenunuliwa dukani.

Ni makosa (ya kisarufi) kusema:

(a)Wanafunzi nane wameingia darasani.

(b)Vitabu visita vimenunuliwa dukani.

Hali sawa na hiyo hudhirika kwenye vivumishi vya sifa. Vivumishi vya sifa hutumika katika sentensi kufafanua maumbile, rangi, au tabia na mienendo ya nomino inayorejelewa.

Vivumishi vyenye asili ya Kibantu kama vile ‘-refu’, ‘-embamba’, ‘-eusi’, ‘-zuri’ na ‘-kubwa’, huchukuwa viambishi awali vya majina vinavyoyaelezea kwa kutegemea ngeli husika ya nomino hizo.

Tofauti

Lakini vivumishi kama ‘rahisi’, ‘madhubuti’, ‘dhaifu’, ‘safi’, ‘hodari’ na ‘kamili’ havichukui viambishi awali vya majina vinavyoyaelezea.

Kwa mfano, tunasema:

“Kisu changu ni kifupi lakini madhubuti”, si “Kisu changu fupi lakini kimadhubuti.”

Tofauti hubainika katika vivumishi vinavyoelezea rangi ya nomino kwani mstari uliopo baina ya vivumishi vipi viwekwe viambishi awali vya majina na vipi visiwekwe, hauna uhusiano na asili ya kivumishi kinachohusika.

Kwa mfano, rangi kama ‘-eupe’, ‘-eusi’, ‘ekundu’ huchukuwa kiambishi cha jina, lakini vivumishi vya sifa kama ‘bluu’, ‘kijani’ na ‘manjano’ havichukuwi sura hiyo. Vinginevyo, makosa ya sarufi hutokea!

[email protected]

You can share this post!

Upinzani wadai wafuasi 30 walionaswa wametoweka

TAHARIRI: Serikali ifikirie upya ufunguzi wa shule