Makala

TAHARIRI: Serikali ifikirie upya ufunguzi wa shule

November 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KITENGO CHA UHARIRI

WIZARA ya Elimu inafaa kufikiria upya msimamo wake kuhusu kufunguliwa kwa shule huku idadi ya maambukizi ya virusi vya corona na vifo ikiendelea kupanda nchini.

Mwishoni mwa wiki jana, kuliripotiwa visa vya wanafunzi kuambukizwa virusi vya corona. Walimu kwenye shule mbalimbali nchini pia wameambukizwa.

Kifo cha hivi punde ni cha mwalimu wa Shule ya Upili ya Olmarai ambaye aliaga dunia katika hospitali ya Nakuru baada ya kupatikana na virusi vya corona. Hiyo inadhihirisha kwamba virusi hivi vimefikia katika shule zetu na huenda wanafunzi wengi zaidi wakaambukizwa.

Mnamo Machi 16 Rais Uhuru Kenyatta aliagiza shule zote zifungwe na wakati huo virusi hivyo havikuwa vimeenea kama sasa hivi hasa baada ya baadhi ya masharti yaliyokuwa yamewekwa kulegezwa. Hatua hiyo ilichukuliwa ili wananchi waendelee na maisha yao kama zamani.

Inasikitisha waziri wa elimu Profesa Magoha ambaye kila mara amekuwa akizuru shule mbalimbali kusema kuwa kuongezeka kwa maambukizi hakutafanya shule kufungwa tena.

Je, waziri anamaanisha kwamba haoni hatari iliyoko shuleni ikizingatiwa baadhi pia sasa hazizingatii masharti kama kunawa mikono, kuvaa barakoa na kuketi umbali wa mita moja unusu?

Kabla ya wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kurejelea masomo yao, alikuwa amenukuliwa akisema shule hazingefunguliwa hadi mwakani kutokana na hatari ya corona.

Sasa tena anasema wanafunzi waliorejelea masomo shuleni hawatasitisha masomo hayo ilhali ni dhahiri walimu wanaambukizwa na kuaga dunia huku wanafunzi nao wakiambukizana.

Hata hivyo, huenda kauli ya Profesa Magoha inatokana na kiburi ambacho kimeonyeshwa na viongozi wetu ambao wamejawa na mapuuza tele. Wengi wao sasa wanaendelea na mikutano yao ya kisiasa kana kwamba virusi vya corona havipo.

Rais Kenyatta anapokutana na magavana na kamati ya kitaifa ya kupambana na virusi vya corona Jumatano, hili suala la watoto kuendelea kusalia shuleni huku maambukizi yakiendelea kufikia kiwango cha hatari linafaa kuangaziwa.

Tayari vyama vya walimu vya Knut na Kuppet vimetoa tahadhari na kutoa wito kwa serikali ifunge shule tena na wanafaa wasikizwe kwa kuwa wapo nyanjani na wanaelewa kinachoendelea.