Makala

MBWEMBWE: Mkwasi huyu wa kutumbua majipu ya wapinzani gozini; usilojua ni alifanya utabibu

November 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

JAMIE Richard Vardy, 33, ni mvamizi matata wa Leicester City na timu ya taifa ya Uingereza.

Upekee wake ni uwezo wa kutamba na mpira katika nafasi yoyote kwenye safu ya ushambuliaji na huwika sana akichezeshwa kama mvamizi mkuu kikosini.

Baada ya kuagana na Sheffield Wednesday akiwa na umri wa miaka 16, Vardy alisajiliwa na kikosi cha Stockbrdge Park Steels mnamo 2007. Alihudumu huko kwa misimu mitatu kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya FC Halifax Town mwanzoni mwa 2010.

Katika msimu wake wa kwanza, alipachika wavuni mabao 25 na kutawazwa Mfungaji Bora wa Mwaka. Ufanisi huo ulimfanya kuwa kivutio kambini mwa Fleetwood Town waliomsajili mnamo Agosti 2011.

Vardy alisajiliwa na Leicester mnamo Mei 2012 kwa kima cha Sh140 milioni. Alisaidia kikosi hicho kutwaa taji la Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) na kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Alivunja rekodi ya Ruud van Nistelrooy kwa kufunga mabao katika mechi 11 mfululizo za EPL na kuongoza Leicester kutwaa ufalme wa taji hilo chini ya kocha Claudio Ranieri.

Mnamo 2019-20, Vardy alifunga mabao 23 ligini na kuweka rekodi ya kuwa mwanasoka mkongwe zaidi kuwahi kutwaa taji la Mfungaji Bora wa Mwaka katika EPL.

UKWASI

Akiwa Stockbridge, Vardy alikuwa akipokezwa mshahara wa Sh4,200 pekee kwa wiki. Japo kwa sasa anapokezwa kitita cha Sh20 milioni kwa juma, thamani ya mali ya Vardy inakadiriwa kufikia Sh2.8 bilioni. Mbali na mshahara huo, Vardy hujipatia hela nyinginezo kutokana na bonasi za kushinda mechi na kusajili sare katika ngazi ya klabu na timu ya taifa. Thamani yake ingaliongezeka zaidi ya mara tano iwapo angalihamia Arsenal mwanzoni mwa msimu mwa 2016-17.

Vardy kwa sasa ndiye anayedumishwa kwa ujira wa juu zaidi kambini mwa Leicester. Mgongo wake kimshahara uwanjani King Power unasomwa kwa karibu na kipa Kasper Schmeichel na kiungo James Maddison.

MAJENGO

Vardy anamiliki kasri la Sh365 milioni mjini Leicestershire, Uingereza. Ana majengo mengine ya thamani kubwa anayotumia kwa shughuli za biashara mjini Sheffield, Uingereza.

MAGARI

Ingawa anajivunia idadi kubwa ya magari, mawili anayoyapenda zaidi ni BMW i3 na 918 Spyder ambayo kwa pamoja, yalimgharimu Sh162 milioni.

FAMILIA

Vardy alianza kutoka kimapenzi na Rebecca almaarufu Becky mnamo 2014 baada ya kukutana kwenye kilabu cha burudani. Wawili hao walifunga pingu za maisha mnamo Mei 25, 2016 katika ukumbi wa Peckforton Castle, Cheshire. Harusi hiyo ilipingwa vikali na wazazi wa Vardy ambao waliisusia. Ana watoto wanne; watatu ambao amezaa na Becky, na mmoja aliyempata katika uhusiano wa pembeni na kichuna mmoja jijini London.

Fowadi huyo pia ni baba wa kambo wa watoto wawili ambao Becky alipata katika mahusiano mawili ya awali na wanaume wengine kabla ya kuanza kumfungulia Vardy mzinga wake wa asali.

BIASHARA

Kabla ya kuwa mchezaji wa kulipwa, Vardy alikuwa mtengenezaji wa vifaa vya kuwasaidia watu wanaovunjika miguu kutembea (crutches). Kwa kuwa alivutiwa sana na taaluma ya utabibu, alipenda pia kuuza dawa pamoja na pamba za kufungia vidonda.

AKADEMIA

Vardy ni mmiliki wa V9 Academy ambayo hutoa mafunzo kwa wanasoka chipukizi ambao hawajapata fursa ya kudhihirisha ukubwa wa vipaji vyao katika ulingo wa soka. Kwa sasa akademia hiyo iliyoasisiwa 2016 nchini Uingereza inajivunia zaidi ya wanafunzi 90 ambao wanapokezwa malezi ya kimsingi kuhusu taaluma ya soka. Akademia hii humvunia Vardy kima cha Sh160 milioni kwa mwezi.

MAAZIMIO

Ingawa aliurefusha muda wa kuhudumu kwake ugani King Power hadi 2023 mwishoni mwa msimu uliopita, matamanio ya mkewe, Rebekah Nicholson, ni kumuona Vardy akivalia jezi za Juventus nchini Italia kabla ya kustaafu soka.

MGOGORO

Vardy aliwahi kuwa katika mgomo baridi na wazazi wake ambao walimpiga vita mpenzi wake Becky, 38, kwa madai kuwa kichuna huyo anamzidi umri kwa miaka mitano.

Vardy alianza kutoka kimapenzi na Becky mnamo 2014 baada ya kukutana kwenye kilabu cha burudani. Wawili hao walifunga pingu za maisha mnamo Mei 25, 2016, katika ukumbi wa Peckforton Castle, Cheshire. Harusi hiyo ilipingwa vikali na wazazi wa Vardy ambao waliisusia.