Matuta yakiwekwa Northern Bypass eneo la Githurai 44 yatasababisha hasara kubwa – Kura
Na SAMMY WAWERU
HALMASHAURI ya Barabara za Mijini (KURA) imesema haitaweka matuta katika barabara ya Northern Bypass eneo la Githurai 44, Nairobi.
Northern Bypass imeunganisha eneo la Ruaka, Githurai, Kahawa West na Ruiru.
Oktoba 17, 2020, wahubiri wa madhehebu mbalimbali eneo hilo walifanya maombi ya pamoja kuondoa mkosi wa ajali katika barabara hiyo, kufuatia ongezeko la visa vya ajali Githurai, makutano ya Kamiti Road na Northern Bypass.
Kulingana na Kasisi wa kanisa la AIPCA, tawi la Githurai, Harison Kimaru, chini ya kipindi cha muda wa miaka miwili pekee eneo la Jordan-Budalangi limepoteza zaidi ya watu 50, ambao wamegongwa na magari.
Bw Kimaru ambaye pia ni mwenyekiti wa mfumo wa Nyumba 10, alisema mapema mwezi Oktoba, mtoto mwenye umri wa miaka 16 alifariki baada ya kupigwa dafrau na gari wakati akijaribu kuvuka barabara.
“Eneo hili ni hatari kwa wakazi, halina matuta, vyuma nguzo za barabara, wala mabango yenye alama za barabara kutahadharisha madereva,” akasema.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Meneja Mkuu wa Mawasiliano Kura, John Cheboi amesema kuweka matuta eneo hilo kutasababisha hasara kubwa.
“Northern Bypass ni barabara yenye shughuli chungu nzima za uchukuzi, muundo wa eneo wakazi wanataka liwekwe matuta haitawezekana. Tukifanya hivyo itakuwa hatari zaidi, kwa sababu huenda yatachangia magari kupoteza mwelekeo na kuelekea kwenye majengo,” Bw Cheboi akasisitiza.
Afisa huyo aliyeonekana kutofautiana pakubwa na kauli ya wenyeji kuhusu idadi ya maafa ya ajali eneo hilo, alisema waathiriwa ni wanaopuuza kuvukia sehemu inayofaa.
Hata ingawa eneo hilo halina daraja maalum la watu – foot bridge – alihimiza wakazi watumie Kamiti Road, barabara iliyopita juu ya Northern Bypass.
“Hata wakazi wenyewe wanachangia hatari, waambie watoto wao wapitie kando (akimaanisha barabara ya juu). Hatutaweka matuta eneo hilo, ni mteremko na ni hatari. Hebu jiulize, lori la kontena limekuja kwa kasi na kuna gari lingine mbele, breki za lori hazifanyi, nini itafanyika?” Cheboi akahoji, akisema barabara hiyo “haina tatizo lolote”.
Barabara ya Kamiti hata hivyo haina nafasi ya watu kupita kwa miguu, jambo linalotia watumizi katika hatari ya kugongwa na magari.
Aidha, alisema wakati wa ujenzi wa Northen Bypass, kandokando hakukuwa na nyumba wala majengo ya watu.
Kuhusu maombi ya kutakasa eneo hilo, Cheboi alisema hakupokea mwaliko, licha ya waandalizi kudai walialika Kura na viongozi waliochaguliwa eneo hilo, akiwemo mbunge wa Roysambu, Waihenya Ndirangu, ila hawakuhudhuria.
Hafla hiyo ilidhuhuriwa na zaidi ya wahubiri 20. Wakazi wanasema Kura pamoja viongozi husika wamekataa kuwapa sikio ili kuangazia ongezeko la ajali na maafa.