Habari

COVID-19: Visa vipya ni 724 huku watu 14 wakifariki

November 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

VISA vipya vya Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita ni 724 kutoka kwa sampuli 5,085 asilimia ya maambukizi ikiwa ni 14.2 ambayo ni ya juu, amesema Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Mgonjwa wa umri wa chini ni mwaka mmoja huku wa umri wa juu akiwa ana umri wa miaka 84.

Watu 14 nao wamefariki kutokana na ugonjwa huo katika kipindi hicho.

Amesema hayo Jumatatu akiwa Malindi, Kaunti ya Kilifi.

“Ninasikitika kwamba katika kipindi cha wiki moja tu tumepoteza zaidi ya watu 100,” amesema waziri Kagwe.

Akaonya: “Tumeanza kupata visa vingi kutoka katika baa, mikahawa na vituo vya huduma za vyakula vya kuchuuzwa hapa na pale. Kuna ukiukaji na upuuzaji wa sheria na mikakati kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu katika maeneo hayo.”

Ongezeko la visa vya corona nchini limeanza kushuhudiwa miezi michache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kulegeza mikakati iliyowekwa mwezi Machi na Aprili 2020 kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Waziri Kagwe ameonya kwamba ukiukaji wa mikakati iliyowekwa ukiendelea, huenda serikali ikatathmini na kurejesha sheria zilizoondolewa kudhibiti msambao zaidi.

“Ombi letu ni kuona kila pahala pakifunguliwa ila mambo yakiendelea tunavyoona huenda tukaweka masharti makali,” akasema.

Kwa wanaotangamana na miili ya waliofariki kutokana na Covid-19, waziri Kagwe amesisitiza haja ya kuwa waangalifu, hasa kwa kuvalia mavazi na vifaa – PPE – kuwazuia kuambukizwa.

“Ninahimiza asasi za usalama kuanzia maafisa wa polisi hadi machifu, mjihadhari na mchunge familia zenu. Mhakikishe mikakati na sheria zilizowekwa zinaheshimika,” akasema.

Huku Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga wakiwa katika mstari wa mbele kuhamasisha umma kuhusu Ripoti ya Maridhiano (BBI) na kurai wananchi kuipitisha endapo kura ya maamuzi kubadilisha Katiba itaandaliwa, waziri amewataka wanasiasa kuheshimu sheria na mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya kukabili corona.

“Kwa wanasiasa, licha ya kuwa tuna suala muhimu tunaloshughulikia, mjue tuna maisha kulinda. Kabla kuandaa mikutano ya umma, mfahamu ugonjwa huu ni hatari,” akahimiza.

Balozi wa Italia Alberto Pieri amesema huu ni wakati ambapo taifa lake limejitolea kuifaa Kenya kukabiliana na ugonjwa huu ambao mara ya kwanza athari zake zilikuwa katika mji wa Wuhan, Mkoa wa Hubei nchini China.

“Italia inajitahidi kuhakikisha kwamba inatoa mchango wake kuifaa Kenya kulikabili janga la Covid-19,” amesema balozi Pieri.

Naye Gavana wa Kilifi Amason Kingi amewataka raia na wageni waendelee kutii masharti, kanuni na maagizo ya serikali kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.