• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Pogba aomba msamaha

Pogba aomba msamaha

Na MASHIRIKA

PAUL Pogba amekiri kwamba alifanya ‘kosa la kijinga’ kwa kumkabili vibaya beki Hector Bellerin katika tukio lililowapa Arsenal fursa ya kufunga penalti na hivyo kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester United.

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Arsenal kusajili dhidi ya Man-United kwenye soka ya Uingereza (EPL) tangu 2004.

Kwa mujibu wa kocha Ole Gunnar Solskjaer, dalili zote katika mechi hiyo ya Novemba 1, 2020, zilikuwa zikiashiria uwezekano wa kukamilika kwa sare tasa kabla ya masihara ya Pogba kuzamisha chombo cha kikosi chake katika dakika ya 69.

Bellerin hakuwa katika nafasi ya kufunga wala kutoa krosi nzuri ya kuchangia bao alipokabiliwa visivyo na Pogba ndani ya kijisanduku. Tukio hilo lilimpa fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang fursa ya kufungia Arsenal kwa mara ya kwanza baada ya mechi tano za EPL.

“Nilikosea sana kwa kumkabili Bellerin kwa namna nilivyofanya. Nilikuwa nimechoka na nikakosa nguvu za kujituma zaidi na kumzuia kutoa krosi,” akatanguliza Pogba.

Akaendelea: “Nilihisi kwamba nilimgusa kifundo cha mguu na nilijua nilikuwa ndani ya kijisanduku, katika eneo hatari. Najutia sana kitendo changu. Hata hivyo, nimejifunza mambo muhimu sasa.”

Penalti hiyo ilikuwa ya tatu kwa Pogba, 27, kusababisha kambini mwa Man-United chini ya kocha Solskjaer. Hakuna mchezaji mwingine ambaye amewahi kusababisha idadi kubwa ya penalti kiasi hicho kambini mwa Man-United.

“Pogba ameungama makossa yake. Anajua kwamba alistahili kujitahidi zaidi kuliko jinsi alivyofanya,” akasema Solskjaer aliyekuwa akiongoza mchuano wake wa 100 tangu apokezwe mikoba ya Man-United.

You can share this post!

Ronaldo arejea ugani kwa matao ya juu baada ya kupona...

Bale afungua upya akaunti yake ya mabao kambini mwa Spurs