Wakili aliyesakwa na ICC ajisalimisha
Na BENSON MATHEKA
WAKILI Mkenya aliyekuwa akisakwa na Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu, (ICC), amejisalimisha kwa mahakama hiyo jijini The Hague, Uholanzi.
Mahakama hiyo ilitoa kibali cha kumkamata wakili Paul Gicheru miaka mitano iliyopita kwa madai kwamba, alishawishi mashahidi katika kesi iliyohusu Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.
Wawili hao walikuwa wamefunguliwa mashtaka kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/ 2008. Hii ilikuwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 ambao walishinda.
Ni kesi hizo zilizowaunganisha wawili hao kwenye uchaguzi huo.
ICC ilitangaza kujisalimisha kwa Bw Gicheru kupitia taarifa Jumatatu ikisema anashukiwa kuhusika na makosa dhidi ya utafutaji wa haki kwa kuwashawishi mashahidi wa mahakama hiyo.
Wakili huyo alitiwa mbaroni baada ya kujiwasilisha katika mahakama hiyo.
“Mahakama, kupitia idara yake ya usajili ilitoa ombi la ushirikiano kwa maafisa wa serikali ya Uholanzi kumkamata na kumwasilisha Gicheru kortini baada ya kukamilisha utaratibu wa taifa hilo wa kutia mbaroni washukiwa,” alisema.
Ofisi ya kiongozi wa mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda ilitoa kibali cha kumkamata Bw Gicheru na mshukiwa mwenzake Philip Kipkoech Bett mnamo Machi 10 2015 ambaye angali anasakwa na mahakama hiyo.
Kulingana na ICC, wawili hao wanalaumiwa kwa kutumia mbinu mbali mbali kushawishi mashahidi waliopaswa kutoa ushahidi katika kesi zilizomkabili Rais Kenyatta na Bw Ruto. Kesi hizo ziliondolewa kwa kukosa mashahidi.
Vibali vya kuwakamata wawili hao vilitolewa Machi 10 2015 lakini havikuwekwa wazi kuwazuia kutoroka au kuvuruga uchunguzi.
ICC ilisema kwamba, haikufichua vibali hivyo hadi Septemba 10, 2015 ili kuzuia wasitishe mashahidi zaidi.
Kulingana na majaji wa ICC, kesi zao zitasikilizwa The Hague kwa sababu wanatilia shaka kujitolea kwa Kenya kuwashtaki wawili hao.
Bi Bensouda alilaumu serikali ya Kenya kwa kutoshirikiana na ICC kuwakamata washukiwa na kutoa ushahidi ambao ungefanikisha kesi za Uhuru na Ruto.