Makala

TAHARIRI: Mpango wa UHC katu usihujumiwe

November 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KITENGO CHA UHARIRI

MAAFIKIANO ya Rais Uhuru Kenyatta na magavana wa kaunti zote 47 kuhusu jinsi ya kufanikisha Mpango wa Afya kwa Wote (UHC), yanafaa kutimizwa kikamilifu ili uweze kunufaisha Wakenya.

Mpango huo ulipokuwa ukifanyiwa majaribio katika kaunti tano nchini, ilibainika kuwa ukilainishwa, unaweza kuwa suluhu kwa tatizo la muda mrefu la ukosefu wa afya miongoni mwa watu masikini nchini.

Changamoto zilizoibuka mpaka ukasitishwa zinafaa kuwa funzo kwa idara husika ili kuufanya uweze kufanikiwa kikamilifu utakapozinduliwa katika kaunti zote nchini. Ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa huduma za afya kwa Wakenya wote ni moja ya Ajenda Nne Kuu za serikali yake, Rais Kenyatta hana budi kuhakikisha masuala yote aliyokubaliana na magavana yatashughulikiwa.

Kufanikiwa na mpango huu, kutamfanya Rais Kenyatta kukumbukwa daima na Wakenya wa kipato cha chini ambao wataathirika ukiyumba au kuyumbishwa na baadhi ya watu wasiotaka ufanikiwe.

Ni wazi kuwa mpango huo umekuwa ukipingwa na watoaji huduma za afya wa kibinafsi ambao lengo lao ni kuendelea kunufaika huku Wakenya wakiendelea kuteseka kwa kutomudu gharama ya matibabu.

Maskini wamekuwa wakilazimika kuuza ardhi kupata pesa za kulipa bili ya matibabu ya wapendwa wao. Wasio na ardhi ya kuuza wamekuwa wakitazama huku wapendwa wao wakifa kwa kukosa matibabu.

Kufaulu kwa mpango huu, kunafaa kuandamana na uboreshaji wa huduma katika hospitali za umma ambazo zinategemewa na Wakenya wa mapato ya chini. Kuwa na mpango mzuri na huduma duni katika hospitali za umma hakutakuwa na manufaa yoyote.

Kabla ya kuzinduliwa kaunti zote nchini, kila hospitali inafaa kuwa na vifaa, dawa na wahudumu wa kutosha wa afya ambao watakuwa wakilipwa kwa wakati kuepuka migomo.

Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu (NHIF) inafaa kusimamiwa vyema ili kuhakikisha kuwa pesa za Wakenya zinalindwa.

Kufaulu kwa UHC kutadhihirika wakati mgonjwa aliye Pokot Magharibi atapata huduma sawa na aliye Nairobi, Mombasa, Mandera na Lamu. Hili linawezekana kukiwa na nia njema na usawazishaji katika utekelezaji wake.

Nia njema itahakikisha serikali kuu itaheshimu maafikiano yake na magavana nao magavana watahakikisha kuwa wakazi mashinani hawatakosa huduma.