• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Guardiola ataka EPL irejeshe kanuni ya kuchezeshwa kwa wanasoka watano wa akiba katika mechi moja

Guardiola ataka EPL irejeshe kanuni ya kuchezeshwa kwa wanasoka watano wa akiba katika mechi moja

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amewataka vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kurejesha kanuni mpya ya kuruhusu jumla ya wachezaji watano wa akiba kuwajibishwa katika mchuano mmoja.

Kwa mujibu wa Guardiola, mrundiko wa mechi ulioshuhudiwa mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 umeshuhudia wachezaji wengi wakipata majeraha mabaya.

“Zaidi ya asilimia 47 ya mejaraha yanayouguzwa na wanasoka wa klabu mbalimbali ni ya misuli. Ina maana kwamba tatizo ni la kuchezeshwa sana uwanjani bila ya kupata muda wa kutosha wa Kupumzika,” akasema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Vikosi vingi vya EPL vilipiga kura ya kukataa kuidhinishwa kwa kanuni hiyo ya kuchezeshwa kwa wanasoka watano wa akiba katika mechi moja msimu huu wa 2020-21.

Sheria hiyo ilipendekezwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ilianza kutekelezwa wakati soka ya EPL iliporejelewa mnamo Juni 2020 baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la corona.

Katika msimu huu, EPL ilirejelea mfumo wa zamani unaoruhusu kila kikosi kufanya hadi mabadiliko matatu pekee katika mchuano mmoja.

Kuhusu haja ya kupunguzwa kwa idadi ya wanasoka wa akiba walio na uwezo wa kuwajibishwa katika mechi moja, vikosi vingine vilihisi kwamba klabu ‘kubwa’ zilikuwa katika hali bora na uwezekano mkubwa zaidi wa kunufaika katika mechi licha ya kanuni hiyo kudumishwa na FIFA na kusalia maamuzi ya klabu za ligi mbalimbali kuamua iwapo zitaendelea kuitekeleza au la.

FIFA ilisisitiza kwamba wachezaji watano wa akiba wanaweza kuchezeshwa katika mechi moja katika mapambano ya hadi Agosti 2021, kumaanisha kwamba kanuni hiyo ipo huru kutumika katika fainali zijazo za Euro na Copa America.

Vikosi vya EPL pia vilipitisha kura ya kuendelea kupangwa kwa wachezaji saba pekee kwenye kikosi cha akiba cha kila timu wakati wa mechi.

Man-City ni Liverpool ni miongoni mwa vikosi vya EPL ambavyo vimelemazwa zaidi na wingi wa visa vya majeraha. Huku Man-City wakilazimika kukosa huduma za Sergio Aguero, Gabriel Jesus, Benjamin Mendy na Nathan Ake kwa muda mrefu, Liverpool wataendelea pia kukosa maarifa ya wachezaji Fabinho, Virgil va Dijk na Joel Matip. Afueni kubwa kwa kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp ni kupona kwa kipa Alisson Becker.

Maoni ya Guardiola yameungwa mkono na kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United, Frank Lampard wa Chelsea na Carlo Ancelotti wa Everton.

IDADI YA MAJERAHA KATIKA EPL:

 

KIKOSI

 

MAJERAHA
Arsenal 5
Aston Villa 3
Brighton 6
Burnley 5
Chelsea 2
Crystal Palace 6
Everton 9
Fulham 6
Leeds United 5
Leicester 6
Liverpool 7
Man-City 5
Man-United 5
Newcastle 5
Sheffield United 4
Southampton 4
Tottenham 2
West Brom 3
West Ham 2
Wolves 1

You can share this post!

Neymar kukaa nje katika mechi tatu zijazo zitakazopigwa na...

Watahiniwa 52 wa KCSE waambukizwa corona shuleni