Bunge kukata rufaa uamuzi kuhusu sheria 23
Na CHARLES WASONGA
BUNGE la Kitaifa linapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutabatilisha sheria 23 lilizopitisha bila kushirikisha Seneti.
Kwenye taarifa kwa wabunge Jumanne alasiri, Spika Justin Muturi alisimamisha kwa muda mijadala kuhusu miswada yote iliyoratibiwa kushughulikiwa na bunge la kitaifa hadi mahakama ya rufaa itakaposimamisha uamuzi wa mahakama kuu.
Mswada wa Kura ya Maamuzi ni miongoni mwa miswada ambayo haitajadiliwa hadi mahakama ya rufaa itakapositisha uamuzu wa kubatilishwa kwa sheria husika.
Hatua hii huenda ikachelewesha ngoma ya Mpango wa Maridhiano, almaarufu kama ‘reggae’ kwa muda.
Bw Muturi alitaja uamuzi huo uliotolewa Alhamisi wiki jana na Majaji Jairus Ngaah, Anthony Ndung’u na Teresia Matheka “usiofaa, yenye nia mbaya na uliokiuka katiba.”
“Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC) ilikutana Ijumaa na kuamua kwa kauli moja kwamba bunge litawasilisha rufaa kupinga uamuzi huo. Vile vile, bunge hili limesitisha mijadala kuhusu miswada yote iliyoratibiwa hadi tutakapopata agizo la kuweka kando uamuzi huo,” akaeleza.
Katika uamuzi wao majaji hao watatu walisema kuwa bunge la kitaifa lilipitisha miswada hiyo bila kusaka idhini ya bunge la seneti inavyohitaji kulingana na kipengele cha 109 cha Katiba.
Hata hivyo, Jairus Ngaah, Anthony Ndung’u na Teresia Matheka waliipa bunge la kitaifa miezi tisa kuafiki matakwa ya Katiba, huku sheria husika zikiendelea kutumiwa.
Jumanne wabunge wakiongozwa na kiongozi wa wengi Amos Kimunya walitaja uamuzi huo kama hatua ya Idara ya Mahakama kuingilia utendakazi wa bunge la kitaifa, hatua ambayo ni hatari kwa uthabiti wa nchini.
Sheria ya Fedha ya 2018 Sheria za Marekebisho ya Sheria za Ushuru ya 2018 (Tax Amendment Laws, 2018) na Sheria inayoruhusu serikali kutumia fedha za umma ya 2018 (Appropriation Bill, 2018) ni miongoni mwa sheria zilizoathirika na uamuzi wa majaji hao.
Sheria ya Fedha ya 2018 ndiyo ilisababisha kampuni ya kamari ya SportPesa kugura Kenya kwa kushindwa kumudu hitaji la kulipa ushuru wa asilimia 20 kutokana na fedha zote ambazo wacheza kamari wangeshinda. Hii ni kando na ushuru wa asilimia 25 ya faida ambao serikali hutoza kampuni zinazoendesha shughuli zao humu nchini.
Ushuru mwingine ulioanzishwa chini ya sheria hii ni ule thamani ya ziada (VAT) ya asilimia 8 kwa bei ya petroli na dizeli ambao ulianza kutumika mnamo Septemba 2018.
Kuanzishwa kwa ushuru huu kulichangia kupanda kwa bei ya bidhaa hizi na hivyo kuwakera watumiaji kwa kupandisha gharama ya maisha.
Mipango ya kuanzishwa kwa ushuru wa VAT kwa mafuta ilikuwa imeahirishwa tangu 2013.
Sheria hiyo pia iliongeza ushuru unaotozwa huduma za kupokea na kutumia pesa kwa njia ya simu kama vile M-Pesa na huduma nyinginezo husika kwa kima cha asilimia 10.
Awali, kampuni ya Safaricom ilikuwa imepinga nyongeza ya ushuru kwa ada zinatozwa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu ikisema hatua hiyo itawaumiza watu wengi masikini, wengi wasio na akaunti za benki na hutegemea huduma za M-Pesa.
Familia zenye mapato ya chini ziliathirika zaidi na kupitia sheria hiyo ya Fedha ya 2018 kwani ilianzisha ada ya Sh18 kwa lita kwa mafuta taa.