Makala

GWIJI WA WIKI: Jane Angila Obando

November 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

KUFAULU maishani na katika taaluma kunahitaji mtu kujituma, kujiamini na kuvuta subira.

Tupo jinsi tulivyo kwa sababu ubora wetu umechangiwa na watu wengine. Hatua ya kwanza katika safari yoyote ya mafanikio ni kufahamu kile unachokitaka, kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda.

Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga, uwe na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika mambo unayoyafanya na uithamini sana familia yako. Jitabirie mambo mema katika siku za usoni na usikubali kushindwa na jambo lolote zuri maishani.

Huu ndio ushauri wa Bi Jane Angila Obando – mwandishi maarufu, mhakiki wa fasihi, mlezi wa vipaji na mwigizaji stadi ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Jane alizaliwa mnamo Novemba 21, 1961 katika kijiji cha Ebulako, Kaunti ya Vihiga. Ndiye wa kumi kuzaliwa katika familia ya watoto kumi na wawili wa marehemu Bi Rumonah Obando na marehemu Bw Nelson Obando.

Mzee Nelson Obando aliyeaga dunia mnamo 1977, aliwahi kuwa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya Ebusakami, Vihiga na Inspekta wa Elimu katika eneo la Kavirondo Kaskazini.

Jane alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Ebusakami mnamo 1967. Alisomea huko hadi darasa la tatu na kujiunga na Shule ya Msingi ya Misikhu Girls, Kaunti ya Bungoma mnamo 1970. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mwishoni mwa 1973.

Alifaulu vyema katika mtihani huo na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Nangina Girls, Kaunti ya Busia kati ya 1974 na 1975. Baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (KJSE), alijiunga na Shule ya Upili ya Tigoi Girls, Vihiga mnamo 1976 na akafanya Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Kidato cha Nne (EACE) mnamo 1977.

Kifo cha baba mzazi kilimtikisa Jane pakubwa na kikatishia kumzimia mshumaa wa elimu ulioning’inizwa kwenye uzi mwembamba wa matumaini.

Alilazimika kusalia nyumbani kwa zaidi ya miaka miwili hadi 1980 ambapo alijiunga na Shule ya Upili ya Matuga Girls, Kaunti ya Kwale kwa minajili ya masomo ya kiwango cha ‘A-Levels’.

Baada ya kukamilisha Mtihani wa Kidato cha Sita (EAACE) mwishoni mwa 1981, Jane alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Hobunaka Boys, Vihiga. Alihudumu huko hadi mwishoni mwa 1983 kisha akajiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Siriba, eneo la Maseno, Kaunti ya Kisumu kusomea Diploma (Kiswahili na Historia) kati ya 1984 na 1985.

Anakiri kwamba maamuzi ya kusomea taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa mno na Bi Kago aliyempokeza malezi bora zaidi ya kiakademia katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Siriba.

UALIMU

Jane aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) mnamo Aprili 1986 na akaanza kufundisha katika Shule ya Upili ya Mbale Boys, Vihiga. Alihudumu huko hadi Januari 2000 alipopata uhamisho hadi Shule ya Upili ya Mutuini Boys, eneo la Dagoretti Kusini, Kaunti ya Nairobi. Ilikuwa hadi Januari 2013 ambapo alijiunga na Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi.

UANDISHI

Uandishi ni sanaa ambayo Jane anakiri kwamba ilianza kujikuza ndani yake tangu alipoanza kuwa mtahini wa kitaifa wa KCSE mnamo 1989. Alitambua makosa mengi yaliyokuwa yakifanywa na wanafunzi katika mitihani na akaazimia haja ya kutunga kazi za kuwasaidia kujibu maswali.

Bi Amina Mlacha Vuzo ni miongoni mwa walimu waliompigia Jane mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na kumpa motisha ya kujitosa kikamilifu ulingoni na kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Jane ameandika ‘Miongozo’ ya vitabu vyote teule vya Fasihi ya Kiswahili ambavyo vimekuwa vikitahiniwa katika shule za sekondari za Kenya tangu 1998.

Ameandika pia vitabu vingi vya mazoezi na marudio kikiwemo ‘KCSE Score More’ alichochapishiwa na kampuni ya Storymoja Publishers jijini Nairobi mnamo 2015.

Zaidi ya ‘Mwongozo wa Insha’, ‘Mwongozo wa Isimujamii’, ‘Mwongozo wa Mashairi’ na ‘Udodosi wa Fasihi Andishi’; msururu wa vitabu ‘Marejeleo Halahala’ katika Sarufi na Matumizi ya Lugha, Isimujamii, Mashairi na Fasihi Simulizi ni miongoni mwa kazi zake nyinginezo. Vitabu hivi vimechapishwa na kampuni ya Nyapunyi Publishers iliyoanzishwa na Jane mnamo 1998.

Jane alikuwa miongoni mwa walimu walioshiriki utunzi wa kitabu ‘Mwandani wa Mwanafunzi’ kilichotayarishwa na Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi mnamo 2015. Kwa sasa anaandaa riwaya ambayo anatazamia ichapishwe hivi karibuni.

DRAMA

Jane alitambua kipaji chake katika sanaa ya uigizaji akiwa mwanafunzi wa A-Levels katika Shule ya Upili ya Matuga Girls. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliowakilisha shule hiyo katika tamasha mbalimbali za kitaifa za muziki na drama na kupata fursa ya kuigiza kwenye majukwaa ya maeneo mbalimbali ya humu nchini.

Mbali na kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi, Jane amekuwa mstari wa mbele kushirikisha wanafunzi wake katika mashindano ya kufyatua filamu na kuigiza. Amewahi kutambuliwa kwenye tuzo za kimataifa za Kalasha zilizoandaliwa katika ukumbi wa KICC mnamo 2015 na akaongoza Moi Girls Nairobi kushiriki drama za kimataifa katika Mkoa wa Lira (2018) na eneo la Fort Portal (2019) nchini Uganda.

JIVUNIO

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Jane amefundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali za maendeleo ya jamii.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo Kiswahili.

Tajriba pevu na uzoefu mpana anaojivunia katika utahini wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuelekeza na kuhamasisha wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa. Ziara hizo zimempa pia majukwaa ya kuhimizana na walimu wenzake kuhusu umuhimu wa kuandika vitabu. Jane anamstahi sana mjukuu wake Rumonah Maloba, 23. Jane anaazimia sasa kuzindua shule ya kimataifa ya mtandaoni ya ‘The International Swahili Mastery Academy’ kufikia Januari 2021.