UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo muhimu katika nadharia ya umilisi wa kiisimu
Na MARY WANGARI
KADRI mwanafunzi anavyozidi kusoma na kujiendeleza kielimu ndivyo kuimarika au kushuka kwa kiwango chake cha umilisi wa lugha kinapozidi kuonekana.
Kiambajengo cha pili ni kuwa, umilisi wa kiisimu huhusishwa na mtu binafsi anayemiliki lugha.
Kila mtumiaji wa lugha husheheni umilisi wa kiisimu wa kipekee ambao ni tofauti na mwenzake.
Mwanaisimu Lehmann anafafanua kuwa endapo watu wawili watajifunza lugha katika mazingira sawa kila mmoja atakuwa na umilisi wa kipekee ambao ni tofauti unapolinganishwa kati ya watu hao wawili.
Umuhimu wa kiambajengo hiki ni kuwa humsaidia mtafiti kuweza kufahamu umilisi wa awali wa kila mwanafunzi au mtumiaji wa lugha husika katika viwango mbalimbali.
Kiambajengo cha tatu kinaeleza kuwa umilisi wa kiisimu huwa na vigezo vya kupimia kiwango katika lugha.
Hii ina maana kuwa umilisi wa kiisimu wa lugha husika yoyote unasheheni vigezo vya kupimia umilisi wa lugha.
Vigezo hivyo ni mapoja na mitihani, majaribio, ufasaha katika mawasiliano na maandishi au matini.
Ufasaha wa mwanafunzi au mtumiaji yeyote wa lugha huweza kupimwa kupitia ujuzi hisa ambacho ni kipimo maalum kinachotumiwa kupima hisa ya umilisi wa lugha.
Jaribio maalum la kiisimu au ukipenda mtihani hupatiwa wanafunzi ambapo majibu yao hukadiriwa na kusaidia katika kutathmini umilisi wa kiisimu wa mwanafunzi.
Mitihani ya lugha ya Kiswahili inaweza kujumuisha uundaji wa sentensi, uchanganuzi wa sentensi mbalimbali kama vile sahili, changamano na ambatano na mengineyo.
Vigezo hivyo vya lugha hutumika kupima umilisi wa kiisimu wa wanafunzi huku watafiti wa Kiswahili wakinufaika kwa data muhimu inayowawezesha kupima umilisi wa kiisimu miongoni mwa wajifunzaji lugha.
Aidha, viambajengo hivyo huwezesha wafundishaji lugha kupima na kuelewa viwango vya umilisi wa lugha miongoni mwa wanafunzi wao.
Nadharia ya motisha na mikabala ya kujifunza lugha ya pili- Nadharia hii iliasisiwa na Gardner (1985).
Mwanaisimu huyu aanaorodhesha vipengele vitatu vinavyojumishwa katika motisha wa kujifunza lugha ya pili.
Vipengele hivyo ni pamoja na: mikabala ya kujifunza lugha, hamu ya kujifunza lugha na kiwango cha motisha.
Marejeo
Lehmann, C. (2006). Linguistic Competence. Erfurt: University of Erfurt.
Massamba, D, Kihore, Y & Hokororo, L . (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI ambayo kwa sasa ni TATAKI
Wanyoike, P. (1978), Vikwazo Katika Mafunzo ya Kiswahili Kenya.