• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umuhimu wa kuzingatia saikolojia unapotunga fasihi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umuhimu wa kuzingatia saikolojia unapotunga fasihi

Na CHRIS ADUNGO

JINSI ilivyo katika sanaa nyinginezo, mvuto ni kitu cha kimsingi sana katika fasihi.

Kipengele hiki cha mvuto ni muhimu zaidi katika fasihi ya watoto na vijana.

Kwa mantiki hii, ili mwandishi aweze kufanikiwa kuiteka saikolojia ya watoto na vijana katika kazi yake ni lazima ahakikishe kazi hiyo inakora saikolojia, masikio na macho ya hadhira yake. Dhana ya mvuto katika fasihi ya watoto na vijana inahusisha vipengele kadhaa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) fasihi ya watoto ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto.

Noun (2010) anasema kwamba fasihi ya watoto ni dhana inayorejelea utunzi unaowalenga watoto pekee. Huweza kuwa hadithi, ushairi, visakale au drama ambazo zimetungwa kwa ajili ya watoto wadogo na vijana. Fasihi ya watoto inajikita katika mambo matatu makuu: Mhusika mkuu lazima awe mtoto, dhamira iwahusu watoto na lugha sahili itumiwe kuendeleza msuko.

Fasili zote hizi zinatupa mwanga hasa juu ya dhana ya fasihi ya watoto na vijana, kwamba ni sanaa inayotumia lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyo chini ya umri wa miaka 18. Dhana ya saikolojia ya watoto na vijana ni yale mambo ambayo yanatakiwa kuzingatiwa katika kazi za fasihi ili kumvutia mtoto na kijana.

Sigh (2002) anasema kuwa fasihi ya watoto na vijana lazima iwe inaonyesha matendo na maisha ya mhusika kinaganaga, mhusika awe anatia hamasa na lazima iwe inaburudisha.

Kwa ujumla, saikolojia ya watoto na vijana katika kazi za fasihi hulenga yale mambo ambayo ni lazima yawepo katika kazi hiyo ili kuwavutia watoto na vijana. Kazi hiyo ni lazima iwe na mtazamo wa watoto. Watoto na vijana wanafikiri tofauti kabisa na watu wazima. Hivyo basi, mwandishi akiandika kazi inayoendana na fikira zao atakuwa amefanikiwa kuiteka saikolojia yao.

Mtoto atakapoona kuwa wahusika wakuu katika kazi ya fasihi ni watoto anaweza kushawishika zaidi kuisoma kazi hiyo kwa hamu ya kutaka kuridhisha matamanio yake.

Watoto hupenda hali ambapo mhusika mkuu huchorwa kama shujaa. Katika kuzikabili changamoto zinazomkumba, mhusika huyo anafaa kuwa kielelezo cha maadili kwa kuonyesha daima uovu ukishindwa na wema.

Ikiwa wazo kuu la kazi hiyo litakosa kuwalenga watoto, basi huenda kwa hakika utunzi huo usipokelewe vyema.

Kazi iwe na lugha rahisi inayoendana na hadhira ya watoto na vijana. Miundo migumu ya sentensi na ploti changamano haipendekezwi kutumiwa katika fasihi ya watoto na vijana isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Mtoto atashawishika zaidi kuendelea kuisoma kazi fulani endapo hatakabiliwa na ugumu wowote wa msamiati na misemo katika usomaji.

Mvuto

Mwandishi anapaswa kuandikia mada inayowavutia watoto na vjiana. Kwa mfano, watoto wengi wanapenda kazi zinazosimulia matukio ya safari. Mwandishi akiandika juu ya mada hizi atakuwa amefanikiwa.

Ni lazima hadithi iwe fupi na ya kiutendaji kwani kazi ndefu huwachosha watoto na hivyo huweza kupoteza mvuto kabisa kwa hadhira.

Mwandishi anapowachora wahusika wake ni lazima kuwe na mhusika mwema na mhusika mwovu kwani hali hii huwavutia sana watoto. Wahusika kama wanyama wapewe uhai na sifa za utendaji. Watoto hufurahia sana wanapoiga sauti na milio ya wanyama mbalimbali.

Pia kazi za fasihi za watoto na vijana sharti ziwe na michezo kwani watoto hupenda sana kunasibishwa na mazingira hayo. Michezo huwafanya wasichoke kusoma hadithi na hivyo kwa njia hii ujumbe utawafikia kwa urahisi.

Kazi iwe na picha, tena za rangi. Hali hii huwafanya watoto kutosahau kwa urahisi kile walichokisoma lakini pia huwasaidia kuhusisha matukio katika hadithi na ulimwengu halisi.

Ni vyema kwa picha zinazotumiwa kuendana na kile kinachosimuliwa. Kwa mfano, picha nyingi zinaweza kuonyesha baadhi ya vitu ambavyo mtoto aghalabu hukumbana navyo katika mazingira yake ya kawaida na ya kila siku. Hali hiyo itamvutia mtoto na apende kuisoma kazi husika.

Taharuki na fantasia pia ni vitu muhimu katika kazi za watoto. Kama chombo muhimu katika fasihi, taharuki itamfanya msomaji wa hadithi aendelee kuizamia zaidi kwa lengo la kujua kile kinachofuatia.

Fantasia huleta mvuto wa kipekee katika fasihi na hivyo kufanya watoto wengi kufurahia sana kazi ambazo huwatoa nje ya ulimwengu wa kawaida.

Kitu kingine kinachowavutia watoto na vijana ni mwisho mzuri wa hadithi. Mwisho wa hadithi unastahili kuibua hisia za furaha badala ya huzuni. Funzo kuu lapaswa kumshajiisha msomaji na kujenga hali ya kujiamini ndani yake anapojitayarisha kukabiliana na ukubwa.

Haya ni mambo muhimu na ya kimsingi ambayo kila mwandishi wa kazi za watoto na vijana anapaswa kuyazingatia pale anapotunga kazi inayowalenga watoto na vijana. Kinyume na hivi watoto na vijana huchukia kazi husika.

You can share this post!

Wakili Gicheru kuishi ‘vizuri’ katika seli ICC

TAHARIRI: Covid: Tusingoje serikali ituokoe