COVID: Uhuru akiri makosa
VALENTINE OBARA na MARY WANGARI
RAIS Uhuru Kenyatta amekubali kuwa mapuuza yake na viongozi wenzake kuhusu janga la corona yamechangia sana nchi kupiga hatua nyuma katika mwezi mmoja uliopita.
Katika hotuba yake kwa taifa Jumatano kuhusu hali ya Covid-19 nchini, Rais alikiri kuwa mikutano ya kisiasa iliyoshamiri katika mwezi uliopita ilichangia ueneaji wa virusi.
atika mwezi huo, viongozi mbalimbali waliandaa mikutano ya hadhara katika pembe tofauti za nchi bila kujali kwamba raia waliokuwa wakiwahutubia walitagusana na wengi hawakuvaa barakoa.
Kando na Rais, mikutano aina hiyo ilisimamiwa na Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, magavana, mawaziri miongoni mwa wengine.
Hii ni licha ya kuwa, serikali ilikuwa imepiga marufuku mikusanyiko ya watu. Hali hiyo ilifanya ionekane kama sheria za kupambana na virusi vya corona hazikuwahusu viongozi wakuu bali walalahoi wanaoadhibiwa vikali kwa makosa kama vile kutovaa barakoa.
Mnamo Jumanne, Dkt Ruto alisimamisha mikutano aliyokuwa amepanga kufanya siku zijazo akisema maambukizi ya corona yameongezeka sana.
“Sisi kama viongozi tumeanguka mtihani kwa sababu tumejifanya ni kama hakuna corona. Kufanya mikutano ya hadhara, kuleta watu bila barakoa na mambo kama hayo yametuumiza,” akasema alipohutubu katika Ikulu ya Nairobi.
Alitoa hotuba hiyo baada ya kukutana na wadau wa Wizara ya Afya na magavana, kuhusu hatua zilizopigwa kufikia sasa na zinazofaa kuchukuliwa kuendelea mbele.
Alijilaumu pamoja na wenzake kwa unafiki, akisema kumekuwa na tabia ya kusema mambo na kutenda vinginevyo.
“Ninawaomba viongozi tuongoze kwa mstari wa mbele. Tusiwe wa kusema na kutenda kivingine. Ni jukumu letu kusema na kutenda yale ambayo tunaambia wananchi wafuate,” akasema.
Katika mwezi wa Oktoba, maambukizi ya virusi vya corona yalipita 15,000 na vifo takriban 300.
Wataalamu wa afya wanaamini hii ilichangiwa na jinsi baadhi ya kanuni za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 zilivyolegezwa.
Katika kanuni zilizotangazwa Jumatano, Rais alijizatiti kuepusha hatua ambazo zingeathiri sana uchumi na shughuli nyingine za kijamii.
Baadhi ya wadau wakiwemo magavana, walikuwa wametoa wito kwa Rais Kenyatta kurudisha masharti makali ambayo yalikuwa yametumiwa wakati ugonjwa huo ulipoingia nchini Machi.
“Mikakati asilia iliyowekwa irudishwe ili kupunguza ueneaji wa maambukizi,” Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Wycliffe Oparanya akasema.
Badala ya kupiga marufuku mikutano ya kisiasa, Rais alisema mikutano itakubaliwa ikiwa itafanywa ukumbini, chini ya kanuni za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo uvaaji wa barakoa.
Katika sekta ya elimu, serikali imeamua shule za msingi na upili zitafunguliwa Januari mwaka ujao.
Hata hivyo, wanafunzi wa Gredi Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne ambao wako shuleni wataendelea na masomo yao wakijiandaa kufanya mitihani.
Wito ulitolewa kwa wabunge kushauriana na bodi za fedha za hazina za maendeleo katika maeneo yao kuboresha miundomsingi ya shule kwa maandalizi ya kupokea wanafunzi wengi.
“Wawekeze katika kuongeza sehemu za kuosha mikono shuleni, kusambaza barakoa, usafi shuleni na kuepusha mtagusano wa wanafunzi na walimu,” akasema Rais.
Serikali pia iliepuka wito wa baadhi ya wananchi kufunga baa ambazo zinaaminika zimechangia ongezeko la maambukizi. Badala yake, Rais aliagiza ziwe zikifungwa saa tatu usiku, sawa na mikahawa.
Wakati huo huo, alitangaza kubuniwa kwa kikosi kipya cha usalama kitakachojumuisha maafisa wa polisi, maafisa wa utawala wa serikali kama vile makamishna na machifu, na maafisa wa usalama wa kaunti.
Kikosi hicho kitahitajika kuhakikisha wananchi hawakiuki kanuni za kupambana na janga la corona.
Rais alitangaza pia kuwa watumishi wa umma walio na umri wa zaidi ya miaka 58 watahitajika kufanya kazi nyumbani, pamoja na wale wanaougua ambao wanaweza kuwa hatarini kuathirika zaidi wakiambukizwa corona.