Michezo

Messi aongoza Barcelona kuwika kwenye UEFA kwa mara nyingine msimu huu

November 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

BARCELONA walisajili ushindi wa tatu kutokana na mechi tatu za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwenye Kundi G baada ya kuwapepeta Dynamo Kyiv ya Ukraine 2-1 mnamo Novemba 4, 2020.

Lionel Messi alifungulia Barcelona ukurasa wa mabao kunako dakika ya tano kupitia mkwaju wa penalti kabla ya beki Gerard Pique kufunga goli la pili katika dakika ya 65 uwanjani Camp Nou.

Messi ambaye ni raia wa Argentina bado hajafungia Barcelona bao lisilokuwa la penalti hadi kufikia sasa msimu huu.

Japo bao la nahodha Viktor Tsygankov lilipania kuwarejesha Kyiv mchezoni katika dakika ya 75, ufanisi huo haukutosha kuwapiku Barcelona waliotamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.

Kyiv walitegemea huduma za kikosi cha wachezaji 13 na chipukizi sita pekee waliosafiri Uhispania kwa minajili ya mchuano huo wa UEFA. Hii ni baada ya wanasoka wao sita kupatikana na virusi vya corona baada ya kufanyiwa vipimo kabla ya gozi hilo.

Barcelona wangalifunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika kipindi cha pili ila wakanyimwa fursa hizo na kipa Ruslan Neshcheret, 18, aliyejituma zaidi na kupangua makombora ya mafowadi wa kocha Ronald Koeman.

Licha ya kwamba Barcelona wameshuhudia matokeo duni katika soka ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu, kikosi hicho kimepania kudhihirisha ubabe wake kwenye soka ya bara Ulaya baada ya kupiga Ferencvaros 5-1 na Juventus 2-0 katika mechi mbili za awali.

Mechi dhidi ya Kyiv iliwapa Barcelona fursa ya kumwajibisha kipa Marc-Andre ter Stegen kwa mara ya kwanza tangu apone jeraha la goti mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba.

Kyiv kwa sasa wanajiandaa kwa gozi kali la Ligi Kuu ya Ukraine dhidi ya Shakhtar Donetsk.

Messi, 33, amefunga bao moja pekee katika mechi sita zilizopita za La Liga; penalti dhidi ya Villarreal.

Rekodi hiyo si nzuri kwa nyota ambaye anajivunia kufungia waajiri wake jumla ya mabao 445 katika kipindi cha miaka 16 ya kuhudumu kwake kambini mwa Barcelona.

Kusuasua kwa Barcelona katika kampeni za La Liga msimu huu kumewashuhusia wakiteremka hadi nafasi ya 12 kwa alama nane kutokana na mechi sita zilizopita.