Rais awataka wabunge watumie mgao wa NG-CDF kuweka mikakati kuzuia watoto na wanafunzi kuambukizwa corona
Na SAMMY WAWERU
SHUGHULI za masomo kwa madarasa yaliyofunguliwa zitaendelea kama ilivyoratibiwa ila kwa kuzingatia mikakati iliyowekwa kuzuia kuenea kwa maradhi ya Covid-19, ametangaza Rais Uhuru Kenyatta.
Chini ya muda wa juma moja lililopita, maambukizi ya Covid-19 yameonekana kuendelea kuongezeka, na licha ya hayo, Rais Kenyatta amesema wanafunzi wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne wataendelea na masomo, huku wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kitaifa wakitakiwa kuendelea kujiandaa.
Wanafunzi wa madaraja hayo walirejea shuleni mwezi uliopita, Oktoba 2020, miezi saba baada ya shule zote na taasisi za elimu ya juu nchini kufungwa kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona.
Kwenye hotuba yake kwa taifa mnamo Jumatano, Rais Kenyatta amesema wataendelea na masomo shuleni, ila kwa kuzingatia vilivyo taratibu na mikakati iliyowekwa kuzuia kuambukizwa ugonjwa huu hatari.
Kiongozi huyo wa nchi aidha amewataka wabunge kutumia mgao wa Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) kuwekeza katika mikakati itakayosaidia kuzuia watoto kuambukizwa corona.
“Kwa wabunge, mtumie NG-CDF kuwekeza katika mikakati kulinda watoto wetu wakiwa shuleni. Mgao huo utumike kununua mashine za kunawa mikono, maski na kuafikia kigezo cha umbali kati ya mwanafunzi na mwenzake,” akaamuru Rais Kenyatta.
Rais Kenyatta ameashiria kuwa wanafunzi wa madarasa mengine watarejea shuleni Januari 2021.
Kauli ya Rais kuhusu wanafunzi waliorejea shuleni kuendelea na masomo, ili kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa iliyoratibiwa kufanyika mwaka 2021, badala ya mwisho wa mwaka huu kama ilivyokuwa katika kalenda ya kawaida, imejiri siku chache baada ya Waziri wa Elimu, Prof George Magoha kusisitiza kwamba shule hazitafungwa licha ya maambukizi ya corona kuonekana kuongezeka kwa kasi.
Ratiba ya mitihani ya kitaifa darasa la nane, KCPE na KCSE 2020 ilisambaratishwa na janga la corona.