Habari Mseto

Blue Nile Rolling Mills yazidi kupiga hatua licha ya janga la Covid-19

November 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Blue Nile Rolling Mills Ltd ya Thika inaendelea kunawiri licha ya changamoto nyingi kipindi cha janga la Covid- 19.

Waziri wa Mauzo na Viwanda Bi Betty Maina, alizuru kampuni hiyo na kuitaja kama mojawapo ya zile ambazo zimejizatiti kujiimarisha.

Alisema licha ya nchi hii kupitia masaibu mengi na kampuni nyingi kufungwa, Blue Nile Rolling Mills ilionyesha ina uwezo wa kujikwamua kutoka kwa changamoto hizo.

“Serikali itafanya juhudi kuiunga mkono kampuni hiyo ili iweze kujizatiti kuendesha biashara yake,” alisema Bi Maina.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi alipozuru kampuni hiyo ili kujionea jinsi imepiga hatua kubwa nchini ya mwaka moja iliyopita.

Alisema kampuni hiyo inaunda vyuma vya ujenzi na vingine vingi vinavyotumika viwandani.

Alitoa wito kwa Wakenya kujizoeshe kununua vifaa vinavyoundwa nchini ili kufuata: ‘Nunua Kenya na Ujenge Kenya’.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kiambu Bi Joyce Ngugi alisema kaunti hiyo itakuwa mstari wa mbele kuiunga mkono kampuni hiyo ili iweze kuafikia malengo yake.

“Kaunti ya Kiambu iko tayari kufanya ushirikiano na kampuni hiyo na viwanda vingine vilivyoko katika kaunti hii,” alisema Bi Ngugi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Blue – Nile Bw Kotni Rao, alisema wameajiri zaidi ya wafanyakazi 800 huku wakiwapa wanawake nafasi ya kwanza katika ajira.

“Tumeweza kutosheleza mahitaji ya wateja wetu kwa kuunda vyema vya viwango vinavyotambulikana na Mamlaka ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs),” alisema Bw Rao.

Alisema kampuni hiyo imewekeza takribani Sh1.9 bilioni huku bidhaa zake zikisafirishwa nchi za nje hasa za bara Uropa na Australia.

Bw Rao alieleza kuwa kampuni hiyo inaunda vyuma vya kiwango cha tani 8,000 kwa mwezi huku kiwango hicho kikiwa kikubwa na kuuzwa nje ya nchi na hapa nchini.

Alisema wanaendelea kujizatiti ili kuimarisha biashara yao licha ya changamoto za Covid-19.

“Tunaelewa virusi vya corona vinaendelea kuenea na kuathiri watu nchini na kwa hivyo wafanyakazi wetu wanafuata sheria zote zilizowekwa na Wizara ya Afya,” alisema mkurugenzi huyo.