Kane afikisha mabao 200 baada ya kuchezea Tottenham mara 300
Na MASHIRIKA
KATIKA mechi yake ya 300 kambini mwa Tottenham Hotspur, fowadi Harry Kane alifunga bao lake la 200 na kusaidia waajiri wake kupepeta Ludogorets Razgrad ya Bulgaria 3-1 kwenye mechi ya Europa League mnamo Novemba 5, 2020.
Ufanisi huo wa kufikisha jumla ya mabao 200 ni jambo ambalo Kane, 27, amesisitiza kwamba hakuwa Kuamini kwamba lingetimia alipoingia katika sajili rasmi ya Spurs miaka saba iliyopita.
Ni wanasoka nguli Jimmy Greaves na Bobby Smith pekee ndio wanaomzidi Kane ambaye huenda akawapita na kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Spurs iwapo atasalia kuchezea kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa muda zaidi.
Akiongoza Spurs kucheza na Ludogorets, Kane aliwaweka waajiri wake uongozini kunako dakika ya 13 kabla ya kuchangia bao lililofumwa wavuni na kiungo Lucas Moura katika dakika ya 32.
Giovani lo Celso alizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao kwa kufungia Spurs goli la tatu katika dakika ya 62.
Bao lililofungwa na Lo Celso lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na fowadi matata raia wa Korea Kusini, Son Heung-min.
Kane kwa sasa anajivunia mabao 200 kutokana na mechi 300. Amefunga magoli 101 kutokana na mechi 135 zilizopita. Kati ya mechi hizo, 100 zimekuwa za ugenini.
Mnamo 1961, Greaves alifungia Spurs mabao 266 baada ya Smith kupachika wavuni mabao 208 kati ya 1955 na 1964 akivalia jezi za kikosi hicho.
Mbali na Kane, wanasoka wengine wa Spurs walioridhisha pakubwa dhidi ya Ludogorets ni Gareth Bale, Steven Bergwijn na Dele Alli.
Mourinho aliwahi kuwaongoza Man-United na ana kiu ya kurejesha kumbukumbu hizo za 2017 akiwatia makali vijana wa Spurs.
Ushindi uliosajiliwa na Spurs dhidi ya Ludogorets ulikuwa wao wa pili ugenini baada ya mechi 10 zilizopita kwenye Europa League.
Kane kwa sasa ndiye mwanasoka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) anayeongoza orodha ya wafungaji bora kutokana na mashindano yote ya hadi kufikia sasa. Nyota huyo amepachika wavuni magoli 12 kutokana na mechi 13 zilizopita.