• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
BAMBIKA: Maceleb wamechoka na tuzo ama kunaendaje?

BAMBIKA: Maceleb wamechoka na tuzo ama kunaendaje?

Na THOMAS MATIKO

KWA miaka mingi tumeshuhudia chimbuko la tuzo mbalimbali za sanaa humu nchini zilizochangia pakubwa kunogesha tasnia yetu ya Showbiz. Iwe ni kwenye muziki au filamu na hata densi, tuzo zimechangia pakubwa kuipa ladha Showbiz ya Kenya.

Miaka ya nyuma, suala la tuzo lilikuwa kubwa sana. Hii ni kwa sababu ziliongeza ushindani kwenye vitengo mbalimbali vya burudani. Wasanii wengi walipambana sana kuhakikisha kwamba nao wanapanda jukwaani kupokea tuzo.

Lakini taratibu kadri miaka ilivyosonga ndivyo navyo tuzo hizi zilianza kupoteza umuhimu wake. Sasa hivi suala la tuzo za ndani haliwashtui wasanii kama ilivyo tuzo za nje. Msanii anapopata mwaliko wa tuzo za ndani na zile za nje, aghalabu atasukuma sana za nje.

Sababu kubwa ya kudidimia kwa tuzo za nchini ni ukosefu wa ufadhili, usimamizi mbaya, mapendeleo na ufisadi kwa ujumla. Makala haya yanakupekechulia baadhi ya tuzo zilizowahi kuwa na msisimko ila sasa hazipo tena au zilikwisha ladha.

KISIMA AWARDS

Baaada ya ukimya wa miaka saba, tuzo hizo zimerejea tena mwaka huu safari hii zikifahamika kama Kisima Music & Films Awards.

Tuzo hizi ziliasisiwa 1994 na maprodusa wakongwe Pete Odera na Tedd Josiah. Licha ya kubuniwa hapa nchini, zilijumulisha mataifa ya Afrika Mashariki. Kwa miaka kadhaa zilizua msisimko mkubwa sana na kunogesha ushindani kwenye muziki. Kufikia 2003 ziliboreshwa zaidi baada ya waandalizi kupata ufadhili kutoka kwa serikali.

Hata hivyo toka 2005, Kisima Awards zilianza kukumbwa na misukosuko jambo lililopelekea kupooza. Kwa mfano kwenye makala ya 2005, Tedd Josiah alishtumiwa baada ya kushinda katika kitengo cha produsa bora. Kama Afisa Mkuu Mtendaji wa tuzo hizo, aliamua kujiuzulu wadhifa wake. Toka hapo kila makala yaliyoandaliwa yalizua utata. Makala ya 2012 yalizua utata hata zaidi baada ya wateuliwa kibao kujiondoa. Tatizo lilianza mara tu baada ya orodha ya majina ya walioteuliwa kuwania vitengo mbalimbali kuzua hisia kali miongoni mwao wasanii, wengi wakidai kulikuwepo na mapendeleo makubwa. Hata mshindi wa makala hayo Daddy Owen aliyeondoka na Sh2 milioni, nusura asusie. Toka wakati huo hazikufanyika tena hadi mwaka huu ambapo zimerejea upya chini ya mfadhili mpya Dkt Fred Simiyu. Makala ya mwaka huu yataandaliwa Disemba 13, 2020 katika hoteli ya Carnivore.

CHAGUO LA TEENIEZ (CHAT) AWARDS

Hizi zilibuniwa 2002 kufuatia mafanikio makubwa na msisimko uliokuwa umeletwa na Kisima Awards. Zilikuwa tofauti, CHAT zilijibidiisha kutambua tasnia tofauti za burudani ambazo zilikuwa zimeachwa nje na Kisima Awards.

Huku Kisima zikiangazia zaidi muziki na wanamuziki, CHAT zilikuja na vipengele vilivyoangazia pia watangazaji bomba wa burudani redioni, maceleb vyuoni, maceleb wakali wa fasheni, wanamitindo na vitengo vingine kama hivyo. Mshindi wa CHAT naye alikuwa akipokea Sh1 milioni. Kwa upana na utofauti huu, CHAT zikaishia kuzua msisimko mkubwa.

Hata zaidi, matineja shuleni wakapewa fursa ya kuhusika kwenye upigaji kura tofauti na ilivyokuwa kwenye Kisima. Hili likasisimua zaidi na mbwembwe za Showbiz zikanoga. CHAT zinakumbukwa kusisimua kwenye mojawapo ya makala yake ambapo rapa CMB Prezzo alikodisha helikopta uwanjani Wilson na kupaa nayo hadi uwanja wa Carnivore ambao ni umbali wa kama mita 800 tu.

Baada ya makala 11 huku kukiwa na chimbuko la tuzo kadhaa, CHAT zilififia na kufa. Aidha sababu kubwa ilitokana na mdhamini mkubwa Fanta, kujiondoa. Zilifufuliwa tena 2020 na kubadilishwa jina sasa zikifahamika kama Chaguo Awards. Hata hivyo zimekosa mashiko. Zikiwa zimesalia siku 11 kabla ya washindi wa vitengo mbalimbali kutangazwa, hamna aliye na habari kuhusu tuzo hizi.

BINGWA MUSIC AWARDS

Ziliasisiwa 2014 na ili kuwa tofauti na zingine, zilijikita kuwatuza wasanii kutoka maeneo mbalimbali. Hichi kilikuwa kitu kipya kwani tuzo za awali ziliangazia zaidi wasanii wa mjini Nairobi.

Licha ya kujitahidi kuleta utofauti, tuzo hizi vile vile zilizua utata. Kwenye makala yake ya 2016, rapa Octopizzo aliyekuwa kakaa kimya kwa muda, alishinda katika kitengo cha ‘Comeback Artist of the Year’. Hatua hiyo ilionekana kumsinya na akaikataa akisema kuwa ilikuwa kumkosea heshima kwa sababu hakuwa ameachana na muziki.

Badala ya kupewa yeye, akapendekeza ipewe Wahu ambaye pia alikuwa amekaa kimya kwa muda kabla ya kurejea na ngoma mpya. Baada ya makala hayo, Bingwa hazijawahi kusikika tena.

GROOVE AWARDS

Baada ya kuchipuka kwa tuzo kibao zilizowatuza wasanii wa muziki wa ‘secular’, 2004 kukabuniwa Groove Awards, ili kuwatunuku wasanii wa injili.

Kwa miaka mingi Groove zimefanikiwa kufanyika hasa baada ya kupata ufadhili na baraka kubwa kutoka kwa kampuni ya Safaricom. Kwenye makala kadhaa yaliyopita, Safaricom ilikuwa ikipiga jeki kwa Sh30 milioni kila mwaka kama mfadhili mkuu.

Zimekuwa zikitolewa kila mwaka toka 2004 sababu kubwa ikiwa ni udhamini. Hata baada ya Safaricom kupunguza ufadhili wake mwaka jana, bado tuzo hizo zilifanyika.

Hata hivyo mwaka huu kumekuwa na ukimya mno hasa ukizingatia kwamba makala ya mwaka jana, washindi walitangazwa mwezi Juni.

MWAFAKA AWARDS

Zilibuniwa kutokana na kuwepo kwa manung’uniko na malalamishi kuhusiana na tuzo za Groove ambapo baadhi ya wasanii wa injili wameishi kudai kuwepo na ubaguzi kwenye uteuzi wa wawaniaji wa vipengele mbalimbali.

Tuzo hizi nazo zikaja na skendo kibao ikiwemo mapendeleo kutoka kwa waandalizi. Hazijakuwa zikifanyika mara kwa mara toka uasisi wake zaidi ya miaka 10 iliyopita. Kwenye makala ya mwaka jana, kulizuka kizazaa baada ya wateuliwa kufika katika ukumbi wa KICC zilikopaswa kufanyika ila wakafurushwa kwa kuwa waandalizi hawakuwa wamelipia eneo kwa mujibu wa maagano.

XTREEM AWARDS

Tuzo hizi zilibuniwa na mfanyibiashara Peter Mulei zaidi ya mwongo mmoja uliopita wakati kukiwa na mgogoro kati ya Groove na Mwafaka. Zimekuwa zikiandaliwa kwa kubahatisha. Baada ya ukimya wa miaka miwili, zilifanyika mwaka jana.

Tuzo hizi nazo zilikuwa za injili ila zilijikita zaidi katika kuangazia vipaji chipukizi tofauti na Mwafaka na Groove zinazoangaziwa wasanii wa injili kwa ujumla. Hata hivyo kama tu Mwafaka, hizi hazina fedha kwa mshindi jambo ambalo imezifanya kukosa mvuto. Licha ya hayo Peter Mulei kaendelea kuhakikisha kuwa hazifi.

You can share this post!

Odera kuongoza wanaraga wa Kenya Simbas kufuzu kwa Kombe la...

Covid: Hofu ya vifo kuongezeka kaunti yatanda